NA SAMMY WAWERU
WAZIRI wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki ameapa kwamba serikali itahakikisha mhubiri tata Paul Mackenzie amehukumiwa kifungo cha maisha
Akitumia maneno “nitahakikisha Mackenzie ataozea jela”, Waziri Kindiki alisema serikali iko tayari kuona pasta huyo anahukumiwa kifungo cha maisha.
Mackenzie hataona mwangaza tena atakaa jela, Prof Kindiki alisema mnamo Jumapili, Juni 4, 2023 akizungumza katika ibada ya misa Kanisa la KAG, Sagana Kirinyaga.
Alitaja kisa cha Shakahola, Malindi, kama mojawapo ya matukio makuu nchini ambayo yamesababisha maafa ya halaiki.
Kufikia sasa, miili 242 imefukuliwa kutoka Msitu wa Shakahola, shamba la Mackenzie.
Pasta huyo wa Good News International Church anatuhumiwa kuhadaa wafuasi wake kufunga bila kula wala kunywaa, kiwaahidi kuwa wakifa wataridhi ufalme wa Yesu.
“Paul Mackenzi atazeekea jela, ataozea jela. Atatoka jela, aende akahukumiwe na Mwenyezi Mungu,” Prof Kindiki alisema.
Waziri akiitaja idara ya mahakama kama asasi ya serikali inayoangusha ile ya usalama, alisema serikali haitachoka kurejesha Mackenzie kortini hadi pale atakapohukumiwa kifungo cha maisha.
Si mara ya kwanza Mackenzie amefikishwa kortini, akiachiliwa huru kwa kile mahakama ilidai kukosa ushahidi wa kutosha kumsukuma jela.
Inahofiwa huenda shamba lake lina makaburi mengi, ya washirika waliofariki katika hali tatanishi.