• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 8:00 AM
Waziri Kindiki: Shakahola ina makaburi mengi

Waziri Kindiki: Shakahola ina makaburi mengi

NA SAMMY WAWERU

ENEO la Shakahola, Kilifi lingali na makaburi mengi, ametangaza Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki.

Kwenye hotuba yake kwa taifa Jumatano, Mei 31, 2023, Waziri amesema shughuli ya ufukuaji maiti zaidi zilizozikwa itaanza Jumatatu ijayo, Juni 5, 2023.

“Makaburi yangali mengi Shakahola na ufukuaji miili utaanza Jumatatu, wiki ijayo,” akasema Prof Kindiki.

Mhubiri tata Paul Mackenzie anahusishwa na suala la Shakahola, mauaji ya halaiki ya wafuasi wake kupitia hadaa za dini na mafunzo potovu.

Kupitia ripoti yake kuhusu hali ya usalama, Waziri Kindiki alisema serikali haitawapa fursa wahubiri wa aina hiyo huku akielezea mikakati iliyowekwa kupiga msasa makanisa na maeneo ya kuabudu.

“Hivi karibuni tutaanza kupiga msasa makanisa na maeneo ya kuabudu ili kujua wachungaji halali na wahuni, ili kuepuka kujipata katika hali tunayopitia waumini kuhadaiwa na mapasta.”

Zaidi ya miili ya washirika 200 wa Good News International Church, kanisa linalomilikiwa na Pasta Mackenzie, imefukuliwa katika shamba lake lenye msitu Shakahola.

Pasta tata huyo analaumiwa kuhadaa wafuasi wake kufunga bila kunywa wala kunywa maji, akiwaahidi hatua hiyo itawafanikisha kuonana na Yesu.

Ripoti ya ukaguzi na upasuaji wa maiti ya miili iliyopasuliwa, inaashiria wengi wa waathiriwa walifariki kutokana na njaa na kukosa maji.

Mackenzie anaendelea kuzuiliwa na polisi, akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya halaiki.

  • Tags

You can share this post!

KAA yasema ‘ajali’ ya ndege iliyoripotiwa...

Madampo kila kona yaharibu sura ya Nairobi

T L