• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
Ziara za Rais ugenini raia wakikaza mshipi

Ziara za Rais ugenini raia wakikaza mshipi

NA BENSON MATHEKA

RAIS William Ruto huenda akaweka historia kama kiongozi wa Kenya aliyefanya ziara nyingi zaidi ugenini iwapo mtindo wake wa sasa wa kusafiri utaendelea.

Kwa miezi minane ambayo amekuwa afisini, Dkt Ruto amefanya ziara zaidi ya 20 nje ya nchi alizoanza siku sita baada ya kuingia ikulu.

Katika mapendekezo ya bajeti ya mwaka ujao wa kifedha, afisi ya rais iliomba Sh2 bilioni za ziara za rais nje ya nchi kuanzia Julai 2023.

Hata hivyo, Wizara ya Fedha ilitengea safari hizo Sh700 milioni ambazo huenda hazitatosha ikiwa rais ataendelea na mtindo wake wa sasa wa kusafiri nje ya nchi.

Ziara yake ya kwanza ugenini ilikuwa Uingereza Septemba 18, 2022, siku sita baada ya kuingia mamlakani alikohudhuria mazishi ya Malkia Elizabeth II.

Baada ya ziara hiyo, rais wa tano wa Kenya alielekea moja kwa moja hadi New York, Amerika kuhudhuria mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA77) ambapo alitoa hotuba yake ya kwanza ya kimataifa akiwa rais.

Mnamo Desemba 6, Dkt Ruto alitembelea Ethiopia ikiwa ziara yake ya kwanza katika nchi za Afrika ambapo alipigania kampuni ya Safaricom kupata leseni ya kuhudumu katika nchi hiyo.

Kwa siku tatu kuanzia Oktoba 8, 2022, hadi Oktoba 10, 2022, Rais Ruto alitembelea nchi mbili majirani, Uganda na Tanzania.

Katika ziara hizi, Rais alifanya mazungumzo na viongozi wenzake kuhusu udumishaji na uimarishaji wa ushirikiano wa kibiashara na kisiasa.

Rais Ruto alirudi Amerika Desemba 14, 2022 kuhudhuria kongamano la Amerika na nchi za bara Afrika lililofanyika jijini Washington D.C.

Mabadiliko ya tabianchi

Ziara nyingine katika nchi ya Afrika ilikuwa Misri mnamo Novemba 6, 2022 kuhudhuria kongamano la 27 la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Wiki mbili baada ya ziara hiyo, alisafiri hadi Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) Novemba 21, kukutana na Rais Felix Tshisekedi kujadili masuala ya biashara na uwekezaji. Taarifa kutoka Ikulu ilisema kwamba viongozi hao wawili pia walijadili masuala yanayohusiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Siku tano baada ya kutoka DRC, Rais Ruto alisafiri hadi Korea Kusini na mnamo Desemba 2, 2022 alizuru Sudan Kusini kabla ya kuelekea Eritrea wiki moja baadaye Desemba 9 ambayo ilikuwa ziara yake ya 10.

Mwezi huo, Desemba 18, 2022, alisafiri hadi Qatar kutazama mechi ya Kombe la Dunia kati ya Argentina na Ufaransa.

Ziara yake ya kwanza nje ya nchi mwaka huu ilikuwa Ufaransa mnamo Januari 24, 2023 kisha kabla ya kufululiza hadi Senegal mnamo Januari 25.

Mnamo Februari 2023, alikutana na Rais Hassan Mohamud wa Somalia katika nchi hiyo jirani kama sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa usalama.

Mwezi huo wa Februari alizuru Burundi( Februari 4) na Ethiopia( Februari 17-19) kabla ya kuelekea Ujerumani mnamo Machi 27 kwa ziara ya siku mbili kisha akaelekea moja kwa moja hadi Ubelgiji.

Mnamo Aprili 2023, kiongozi wa nchi alizuru Rwanda (Aprili 4- 5) na Uganda (Aprili 26).

Kwa wiki moja kuanzia Mei 6 hadi Mei 10, Rais Ruto alikuwa katika ziara Ulaya iliyompeleka Uingereza kushuhudia kutawazwa kwa Mfalme Charles III, Uholanzi kabla ya kutembelea Israeli. Alirejea Mei 10 na baada ya wiki moja akazuru Afrika Kusini.

Katika ziara hizo, Rais Ruto amekuwa akifanya mazungumzo na kutia saini mikataba ya kufanikisha biashara, utalii, kukabili mabadiliko ya tabia nchi na kufungua milango ya uwekezaji nchini.

Iwapo ziara zake zitaendelea, atakuwa amefuata nyayo za mtangulizi wake Uhuru Kenyatta ambaye alitumia mabilioni ya pesa kutembelea nchi tofauti.

Rais wa nne wa Kenya Mwai Kibaki anayesifiwa kwa kukuza uchumi alifanya ziara 33 nje ya nchi kwa miaka kumi aliyokuwa mamlakani.

Ziara za kiongozi wa nchi huwa zinagharimu mamilioni ya pesa ikiwa hazidhaminiwi na nchi anayotembelea.

  • Tags

You can share this post!

Thugge kuondoa sheria inayozuia Wakenya kuweka na kutoa kwa...

Akaunti za M-Pesa za Pasta Ezekiel Odero zafunguliwa...

T L