• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 9:55 AM
Aina mpya hatari ya corona yagundulika

Aina mpya hatari ya corona yagundulika

Na ELIZABETH MERAB

WANASAYANSI wanachunguza kuhusu mchipuko wa virusi vipya vya corona aina ya Delta, katika nchi za Amerika, Uingereza, Urusi na Israeli.

Virusi hivyo vinaitwa AY.4.2. Hilo linajiri siku kadhaa baada ya Kenya kuondoa baadhi ya masharti iliyokuwa imeweka kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

Miongoni mwa masharti yaliyoondolewa ni kafyu, iliyokuwa ikitekelezwa kati ya saa nne usiku na saa kumi alfajiri.

Vile vile, serikali ilitangaza kuondoa masharti yaliyokuwepo kuhusu mikusanyiko ya watu katika maeneo mbalimbali ya umma.

Serikali ilitangaza kuondoa masharti hayo baada ya Kenya kufanikiwa kukabili wimbi la nne la maambukizi.

Alhamisi, Kaimu Mkurugenzi wa Afya, Dkt Patrick Amoth, alisema kwamba ijapokuwa virusi bado vinaendelea kuwepo nchini, Wizara ya Afya inafuatilia kwa kina msambao wa virusi aina ya AY.4.2.

“Licha ya nchi kama Uingereza kufanikiwa kutoa chanjo kwa idadi kubwa ya raia wake, inaendelea kukabiliwa na athari za aina hiyo ya virusi. Tunafuatilia kwa kina mwelekeo wake kwani unaweza kuvuruga taratibu zetu za utoaji chanjo,” akasema Dkt Amoth.

Kwa miaka miwili iliyopita, virusi hivyo vimekuwa vikibadilisha muundo wake. Kulingana na wataalamu, vimeanza kusambaa nchini Uingereza na vimethibitishwa kuwepo Amerika, Urusi na Israeli.

Ingawa aina hiyo ya virusi ni nadra, wataalamu wanaifuatiliwa kwa kina, kwani vimebainika kuwa chanzo kikuu cha ongezeko la visa vya maambukizi.

Aina hiyo imetajwa kujumuisha asilimia kumi ya visa vyote vipya vya maambukizi vinavyobainika.

Kulingana na Profesa Walter Jaoko, ambaye ni Mkurugenzi wa Mpango wa Kenya kuhusu Chanjo ya Ukimwi (KAVI), bado ni mapema kubaini muundo mpya wa aina hiyo ya virusi.

“Kuna mengi ambayo bado hatujui, kwa mfano sababu zinazoifanya aina hiyo kuwa hatari zaidi ikilinganishwa na aina zingine,” akasema Prof Jaoko, ambaye ni mtaalamu wa maradhi ya kuambukizana.

Hata hivyo, mtaalamu huyo anasema Kenya inapaswa kuwa katika hali ya tahadhari, kwani haijabainika ikiwa virusi hivyo vimefika nchini au la.

“Hapa nchini, ni vigumu kubaini ikiwa virusi hivyo vimefika kwani bado hatuna mashine za kisasa. Kuna maswali mengi ambayo bado hayana majibu,” akasema.

You can share this post!

Matiang’i atisha kufunga vyombo vya habari vinavyotumika...

Zaidi ya vyuo 500 vya udereva hatarini kufungwa

T L