• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
Akaunti za Pasta Ezekiel Odero kufunguliwa

Akaunti za Pasta Ezekiel Odero kufunguliwa

Na RICHARD MUNGUTI

MHUBIRI Ezekiel Ombok Odero wa Kanisa la New Life Church and Prayer Center, ana kila sababu ya kutabasamu baada ya mahakama kuamuru polisi kufungua akaunti zake za benki na M-pesa.

Hakimu mkazi Mahakama ya Milimani Ben Mark Ekhubi aliagiza Jumatatu, Mei 22, 2023 akaunti za pasta huyo zifunguliwe aendelee na harakati za kufadfhili elimu ya wanafunzi 3, 000 wa Kilifi International School.

Wakili Danstan Omari anayemwakilisha Odero alimweleza hakimu “pesa zilizofungiwa ni za waumini wa kanisa na wala sio za pasta.”

Sasa Mchungaji Odero yuko huru kufika katika benki za Cooperative, KCB na NCBA kupata pesa.

Huku polisi wakiagizwa wafungue akaunti za Bw Odero, hakimu alimwamuru afisa mkuu wa masuala ya sheria wa kampuni ya Safaricom afike kortini Mei 30 kueleza sababu za kutoruhusu polisi kuchunguza mitandao saba za M-Pesa za pasta huyo.

Kukamatwa na kuzuiliwa kwa wakazi wa kisiwa cha Ngodhe katika Ziwa Victoria wangali wamepigwa na butwaa kuhusiana na masaibu yanayomkumba mwana wao, Mhubiri Odero.

Alizaliwa na kukulia kisiwani hapo kabla ya kuhama na kwenda kueneza injili Kaunti ya Kilifi.

Anachunguzwa kwa msururu wa mashtaka yakiwemo ya ulaghai, utakataji wa fedha, mauaji, utoaji wa mafunzo ya itikadi kali, unyanyasaji wa watoto miongoni mwa mengine.

Wakati wapinzani wake wanaendelea kusema mengi juu yake, nyumbani mtumishi huyo wa Mungu ana heshima kubwa kutokana na msaada wake wa watu wa kwao.

Wakili Danstan Omari anayemwakilisha Pasta Ezekiel Odero. Picha / Richard Munguti

Anafahamika vizuri kwa jina la Ombok.

Wavuvi katika kisiwa hicho wana historia kubwa juu ya mtu huyu ambaye alikuwa akitoka nao usiku kwenye safari za uvuvi ili aweze kuongeza kile ambacho wazazi wake wangeweza kutoa kwa familia yao kabla ya nyota yake kumwangazia.

Ili kufikia Kisiwa cha Ngodhe kusema na jamaa wake, tuliabiri boti yenye injini na ilituchukua takriban dakika 20 kabla ya kutia nanga. Kisha tukapanda vijiji vya milimani kabla ya kufika wanakoishi wazazi wake.

Tulipowasili kwo mchungaji Ezekiel, tulivutia umati mkubwa wa watu uliokuja kusikiza kilichotupeleka pale.

Nyumba ya wazazi ni kubwa na ndani imetengenezwa vizuri.

Wengi wa watu hawa walikuwa wavuvi ambao walipoona kamera zetu, walikuwa na wasiwasi na walitaka kujua ni nini kilikuwa kimetupeleka katika “eneo” lao.

Baada ya kuwaeleza, walituongoza hadi bomani.

Ikilinganishwa na nyumba ya wazazi wake, ya Mchungaji Ezekiel ni ya bei nafuu.

Imejengwa kwa mabati ya kawaida na kuta zake ni za saruji.

Inasimama kwa kutengwa mita chache kutoka kwa ile ya wazazi lakini imejisitiri katika kiwanja kilichookotwa majani vizuri.

Ili kuingia kwa mchungaji, unapaswa kupitia lango rahisi linalotenganisha nyumba ya wazazi na yake.

Hakimu Ben Mark Ekhubi. Picha / Richard Munguti

Tulikaribishwa vyema na mamake, Bi Rebecca Odera sebuleni.

Sekunde chache baadaye, babake mchungaji Ezekiel alijiunga nasi kisha jamaa wengine wakafuata.

Waliingia mmoja baada ya mwingine mpaka viti vyote vya sebuleni vikakaliwa.

Wazazi wa Ezekieli walionekana kuchoka. Walikuwa wavumilivu sana na ingawa hawakuzungumza mengi kuhusu mtoto wao, wavuvi waliotufuata nyumbani walifunguka.

“Ombok alilelewa katika malezi duni na alizoea kuungana nasi usiku tulipokuwa tukienda kuvua samaki. Hakuwa na chaguo lingine isipokuwa kuongeza kile ambacho wazazi wao wangeweza kutoa kupitia uvuvi,” binamu ya Pasta Ezekiel, Alfred Oketch alisema.

Miaka ya 1990, Bw Oketch alikumbuka jinsi walivyokua pamoja na Ombok.

Alidai kuwa walipokuwa wakienda katika Kanisa la Waadventista Wasabato Kisiwani Ngodhe, Mchungaji Ezekiel alipenda sana kufunga kisha kubaki nyuma kwa ajili ya maombi waumini wengine walipokuwa wakienda nyumbani kwa chakula cha mchana.

“Alikuwa akibaki nyuma na kuzama kwenye sala. Angeweza kuimba sana katika kwaya ya kanisa na wakati fulani alikuwa mwalimu wa kwaya yetu. Baadaye, aliondoka kijijini kisha akaenda Mombasa ambako alianzisha kanisa lake,” Bw Oketch aliongeza.

Tangu alipoondoka kwenda Pwani kulingana na Bw Oketch, Ombok hakuwasahau watu wake.

“Analipa karo kwa wanafunzi wengi hapa kisiwani Ngodhe, watoto wangu wakiwemo. Tunamfahamu kuwa mtu mkarimu na dhiki anazopitia kwa sasa zimetushtua,” Bw Oketch alisema.

Maoni sawa na hayo yalitolewa na Bw Kennedy Odero, ambaye aliangazia baadhi ya miradi katika kijiji chao ambayo alisema Ombok alikuwa akifadhili.

Hii ni pamoja na Shule ya Msingi ya Ngodhe alikokwenda kwa ajili ya masomo yake ya utotoni na Kanisa la Waadventista Wasabato

“Kila tulipokuwa tukienda kwenye mikutano ya kambi, yeye ndiye alikuwa akilipia bili zetu na gharama nyingine zote zinazoongezeka. Vipaza sauti tunavyotumia vilinunuliwa na Ombok na tunamshukuru kwa ishara nzuri,” Bw Kennedy aliongeza.

Walipoombwa waseme jambo fulani kuhusu mwana wao, wazazi hao waliamua kutozungumza.

“Mungu afanye kazi yake, kama serikali inavyofanya yao. Ndivyo tunaweza kusema,” walisema kwa pamoja.

Babake Ombok alisema walichagua kutozungumza sana kwa sababu kwa kufanya hivyo, watu wengi wangewahukumu na kusema kwamba wanawatetea mwana wao.

Kisii, kakake mdogo Mchungaji Ezekiel Gillack Odero, amefungua tawi lingine la Kanisa la New Life eneo la Itibo-Rianabaro, mita chache kutoka mji wa Suneka.

Anasimamia hapa na ukimuuliza kuhusu anachopitia kaka yake, inamuuma sana lakini anajikusanya na kusema jambo.

Ingawa Mchungaji Ezekiel ni kaka yake wa damu, Gillack anamtaja kama babake wa kiroho na kusema kwamba alimpa baraka zake zote alipomweleza matamanio yake ya kufungua tawi lingine la Kanisa la New Life Church Kisii.

Mchungaji Gillack pia huvaa vazi maarufu jeupe ambalo kaka yake huvaa.

Akielezea kuhusu sarakasi iliyohusisha ndugu yake, kasisi Gillack alilinganisha kisa cha ndugu yake na aina ya dhiki ambayo Yesu alipitia alipokuwa duniani. Walakini, alijiamini kuwa watashinda.

Yeye pia alifichua kwamba kama kaka yake, akaunti zake za benki zilikuwa zimefungwa lakini aliamini kwamba hatimaye, mapenzi ya Mungu yatatawala.

“Tunamtumikia Mungu aliye hai. Mimi na kaka yangu tumetoka mbali na tumeuona mkono wake. Ni wale tu ambao wameona tuliyopitia kabla ya kufika tulipo wanaweza kuelewa ninachosema,” mchungaji Gillack alisema.

Alifichua kuwa hivi karibuni kanisa lake litahama kutoka Rianyabaro hadi eneo kubwa zaidi Kaunti ya Kisii.

Wale wanaohudhuria ibada yake wanatoka mbali kama Migori kwa ajili ya kulishwa kiroho.

  • Tags

You can share this post!

Mbappe abeba PSG dhidi ya Auxerre

Masaibu ya mhubiri Ezekiel yasikitisha wakazi Ngodhe

T L