• Nairobi
  • Last Updated June 1st, 2023 12:23 AM
Amerika, EU waonya wanajeshi wa Sudan dhidi ya kutwaa uwaziri mkuu

Amerika, EU waonya wanajeshi wa Sudan dhidi ya kutwaa uwaziri mkuu

Na AFP

AMERIKA, Uingereza, Norway na Umoja wa Ulaya (EU) zimeonya vikali wanajeshi wa Sudan dhidi ya kuteua mwanajeshi kuwa waziri mkuu kufuatia kujiuzulu kwa kiongozi wa kiraia Abdallah Hamdok wiki iliyopita.

Mataifa hayo, kupitia taarifa ya pamoja, jana yalisema kuwa hayataunga mkono waziri mpya iwapo atakuwa mwanajeshi.

Mataifa hayo yalitoa wito wa kuendelea kwa maandalizi ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Julai, 2023.

Taarifa hiyo iliyotolewa na wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika, iliwataka viongozi na kiraia na wanajeshi kuanza mazungumzo mara moja ili kutatua masuala tata yanayohusiana na serikali ya mpito.

Nchi hizo zilisema kuwa zingali zinaamini makabidhiano ya madaraka kutoka kwa wanajeshi kwa njia ya kidemokrasia yatafanyika.

Mataifa hayo yenye utajiri mkubwa yalitishia kuchukua hatua kali dhidi ya jeshi la Sudan endapo litajinyakulia mamlaka na kukosa kuhusisha raia.

Hamdok alijiuzulu wiki sita baada ya wanajeshi kumrejesha mamlakani Novemba, mwaka jana. Hamdok alipinduliwa Oktoba baada ya wanajeshi kumzuia kuondoka nyumbani kwake kwa wiki kadhaa.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Amerika Ned Price alisema taifa hilo bado linaamini katika makubaliano ya mwaka 2019 yaliyofikiwa kati ya waandamanaji na jeshi lililomuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo Omar al-Bashir mnamo Aprili 2019.

Kwenye taarifa hiyo, mataifa hayo pia yameelezea wasiwasi wao kuhusiana na hatua za jeshi dhidi ya waandamanaji yakisema raia wana haki ya kuandamana.

Watu zaidi ya 60 wameuawa tangu wanajeshi kujaribu kupindua serikali ya Hamdok mnamo Oktoba, mwaka jana.

“Hatutasita kuwaadhibu watu watakaotatiza mchakato wa kuhakikisha kuwa Sudan inarejea katika mfumo wa demokrasia,” ikasema taarifa ya mataifa hayo.Mataifa ya Magharibi yalikuwa yakiunga mkono Hamdok ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi wa Umoja wa Mataifa (UN).

Hamdok alisomea nchini Uingereza.Kuondoka kwa Hamdok ni pigo kubwa na huenda taifa hilo likaingia kwenye mzozo mkubwa zaidi.

Maelfu ya raia wa nchi hiyo wamekuwa wakiandamana katika juhudi za kushinikiza wanajeshi kukabidhi mamlaka kwa raia. Hamdok alijiuzulu kutoka wadhifa wa waziri mkuu Jumapili huku akisema kuwa maisha yake yalikuwa hatarini.

“Harakati za kuongoza nchi kutoka kwa utawala wa kijeshi hadi uongozi uliochaguliwa na wananchi zinafaa kuendeshwa na raia na wala si wanajeshi.“Waziri mkuu mpya wa Sudan anastahili kukubalika na raia wote wa Sudan,” akasema Price.

Mataifa hayo pia yalionya wanajeshi dhidi ya kuingilia mchakato wa kuteua mawaziri watakaoendesha nchi hiyo wakati wa kipindi cha mpito.

“Jeshi halina budi kushiriki kwenye mazungumzo yatakayoongozwa na jamii ya kimataifa kujadili masuala tata yanakumba nchi kipindi hiki cha serikali ya mpito,” akasema.

Mataifa ya magaribi yalionya wanajeshi dhidi ya kutawanya raia ambao wamekuwa wakiandamana huku yakisema kuwa wananchi wana uhuru wa kutoa malalamishi yao na wanastahili kulindwa.

  • Tags

You can share this post!

Mgomo wa matrela waingia siku ya nne

Hasara tele wanabiashara wakitorokea eneo salama kutokana...

T L