• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Bobi Wine alia njaa majeshi yekiendelea kumfungia nyumbani mwake

Bobi Wine alia njaa majeshi yekiendelea kumfungia nyumbani mwake

Na DAILY MONITOR

KAMPALA, Uganda

MAAFISA wa usalama Jumatano waliendelea kuzingira makazi ya aliyekuwa mgombeaji wa urais wa upinzani Uganda Robert Kyangulanyi siku tano baada ya Rais Yoweri Museveni kutangazwa mshindi katika uchaguzi mkuu wa Januari 14.

Mwanasiasa huyo, maarufu kama Bobi Wine, sasa analalamikia kuishiwa na chakula na mahitaji mengi huku balozi wa Amerika akizuiwa kumtembelea.

Jumanne jioni Balozi Natalie Brown ambaye alifika kijiji cha Magere, wilaya ya Wakiso ambako Wine amewekwa chini ya kifungo cha nyumbani lakini akazuiwa na maafisa wa polisi na wanajeshi walipokaribia makazi yake.

Baadaye msemaji wa polisi Fred Enanga alihoji hatua hiyo na kile alichotaja kama kuhusika kwa Amerika katika siasa za ndani za Uganda.

“Amerika ina nafasi gani katika siasa za nchini hii? Je, balozi wa Amerika ana uhusiano wowote wa kibinafsi na Mheshimiwa Kyangulanyi. Hiyo inaibua shauku nyingi, alienda kufanya nini huko?” Bw Enanga akauliza usiku wa kuamkia jana.

Wakati wa kampeni, Rais Museveni alimtaja Wine kama kibaraka cha “taifa moja la kigeni.”

Lakini ubalozi wa Amerika ilijibu, kupitia barua pepe iliyotumwa na msemaji Anthony Kujawa, kwamba “nia ya ziara ya Balozi Brown ilikuwa ni kuchunguza afya na usalama wa Robert Kyangulanyi. Hii ni kwa sababu hajaweza kuondoka nyumbani huku maafisa wa usalama wakizingira makazi hayo wakidai wanampa ‘usalama’ ambao hakuomba.”

You can share this post!

Trump aacha Amerika yenye aibu na ubaguzi

Demokrasia imeshinda, asema Biden baada ya kuapishwa kuwa...