• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 10:30 AM
Bobi Wine ashambuliwa kwa madai yake kuhusu sheria ya ushoga Uganda

Bobi Wine ashambuliwa kwa madai yake kuhusu sheria ya ushoga Uganda

NA MASHIRIKA

KAMPALA, UGANDA

MWANASIASA wa Uganda Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine, amekosolewa vikali kwa kudai kwamba Rais Museveni alipitisha sheria tata kuhusu ushoga ili kumlenga yeye.

Mwanasiasa huyo akiwa Uingereza, alisema wabunge wa chama chake cha National Unity Platform (NUP) ambao waliunga mkono sheria hiyo, ‘wanashirikiana na Jenerali Museveni’.

“Nataka kusema kwamba sheria hii, Jenerali Museveni hakuileta kwa maslahi ya watu wa Uganda. Lakini ililetwa kulenga Upinzani, ikiwa ni pamoja na mimi. Hii ni kwa sababu anataka kutumia sheria hiyo kukandamiza mtu yeyote ambaye anaonekana kuwa rafiki kwa jamii hiyo (mashoga),” Bobi Wine alisema katika mahojiano.

Alijibu hayo baada ya kuulizwa kwa nini chama chake kilipiga kura kuunga mkono mswada wa kuharamisha ushoga Uganda.
“Hakika! Katika chama changu nina wabunge wanaofanya kazi na Jenerali Museveni”.

Hata hivyo, Bobi Wine hakutoa ushahidi wowote kuthibitisha madai yake na hakutaja hata mmoja wa wabunge hao.

Bobi Wine alitoa maoni hayo kwa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) mnamo Novemba 29 wakati wa ziara yake ya kwanza London, miaka kumi baada ya serikali ya Uingereza kumzuia kwa maoni yake kuhusu ushoga.

Jijini Kampala, Chama cha Upinzani cha JEEMA kinachoongozwa na Asuman Basalirwa na ndicho kilichofadhili sheria ya kupinga ushoga, kilimkashifu Bobi Wine kwa matamshi hayo.

“Unafahamu sheria ya kupinga ushoga ililetwa na Asuman Basalirwa, kiongozi wa JEEMA na iliendana na kile tunachokiamini kama JEEMA. Sheria hii iliungwa mkono kwa kiasi kikubwa na Bunge zima, (ikiwa ni pamoja na)wabunge wa NUP ambao walihatarisha maisha yao ili kulinda maadili yetu ya kitamaduni na kidini,” Katibu Mkuu wa JEEMA Mohamed Kateregga alibainisha katika barua iliyoelekezwa kwa Bobi Wine.

  • Tags

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Maadili yako wapi, tunafunza nini...

Wasiwasi waibuka Embu watu 15 wakijitoa uhai ndani ya miezi...

T L