• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 7:55 PM
COP28: Wanaharakati wakubaliwa kuandamana kupinga matumizi ya visukuku, machafuko Gaza

COP28: Wanaharakati wakubaliwa kuandamana kupinga matumizi ya visukuku, machafuko Gaza

NA JACOB WALTER

Akiwa DUBAI, UAE

HATIMAYE wanaharakati wamekubaliwa kuandamana jijini Dubai katika Milki za Kiarabu (UAE) ili kutoa malalamishi yao kuhusiana na michakato kadhaa inayojadiliwa kwenye kongamano la Umoja wa Mataifa la COP28.

Maandamano yalianza Jumamosi ambapo wakereketwa wa haki za kibinadamu walitaka ukomeshaji wa mauaji ya raia wa Palestina katika eneo la ukanda wa Gaza katika uvamizi ambao umekuwa ukiendelezwa na Israel dhidi ya Hamas.

Aidha, Jumapili wanaharakati kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Kenya, walihanikiza sauti zao wakitaka utekelezwaji upesi wa ukomeshaji wa uchafuzi wa hewa na mazingira unaoendelezwa na mataifa tajiri duniani.

Maandamano hayo yamefanyika pia Jumatatu asubuhi.

Wakibeba mabango yalioandikwa ‘no more fossil fuels’ kumaanisha hukupswi kuwepo tena kwa mafuta ya visukuku na ‘let Lake Victoria Breathe Again’ kumaanisha ‘acha Ziwa Victoria lipumue tena’, wanaharakati hao walipata nafasi ya kuelezea malalamishi yao kwa umma kwa muda wa saa moja.

Akiongea na Taifa Leo, mwanaharakati na Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika la Eurogroup for Animal tawi la Kisumu Miriam Wanjiku ameeleza kuwa wanaharakati hao walilazimika kupaza sauti zao kulalamikia kile walisema ni misimamo isiyoaminika kuhusu kupigwa marufuku kwa aina za kawi zenye athari kubwa kwa uchafuzi wa mazingira.

Amesikitika kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zimeendelea kufanya maisha kuwa magumu zaidi kwa mataifa maskini.

“Nasikitika kuwa mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuathiri pakubwa wananchi hohehahe katika mataifa ambayo ndiyo yanajaribu kuinukia kama Kenya ilhali hawapati fidia. Hii ndiyo sababu yetu kusisitiza kuwa sharti waathiriwa sasa wapate fidia na pia ni sharti mataifa yote yakome kutumia kawi ya visukuku,” akaeleza Bi Wanjiku.

Mwanaharakati wa mazingira na Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika la Eurogroup for Animal tawi la Kisumu Miriam Wanjiku akiandamana jijini Dubai katika Milki/Falme za Kiarabu (UAE). PICHA | JACOB WALTER

Maisha ya viumbe hai yameendelea kudorora kutoka kwa binadamu ,wanyama na miti na mimea mingine kutokana na uchafuzi unaoendelezwa na nchi zinazojiweza kiuchumi kupitia kwa gesi zenye sumu kama hewa ukaa na vichafuzi vinginevyo kulingana na mwanaharakati huyo.

Alitoa mfano wa jinsi Ziwa Victoria linavyozidi kuchafuka na kusababisha hata aina za samaki waliojulikana kwa muda mrefu, kuanza kudidimia kwa kasi mno.

Mifumo yote ya maji kama maziwa, bahari, chemchemi na mito imeathirika pia, huku maisha ya viumbe hai yakiwa taabani.

Kaulimbiu yake katika maandamano ni ‘Ruhusuni Ziwa Victoria kupumua tena’.

Aidha Bi Wanjiru amesikitika kuwa maisha ya mianzi ya matumbawe (coral reefs) katika Bahari Hindi pia ni ya kuzua hofu akisema kuwa uchafuzi wa mazingira ndio wa kulaumiwa.

Haya yanapojiri, baadhi ya wanasayansi kutoka Kenya pia wameeleza kutoridhishwa kwao na hatua zilizochukuliwa na mataifa yanayojiweza katika ukomeshaji wa matumizi ya kawi ya visukuku (fossil fuel).

Amesikitikia sana kuongezeka kwa majanga yanayosababishwa na tabia nchi kama mafuriko na ukame yameendelea kuongezeka katika bara la Afrika.

Amesikitika kuwa hatima ya vizazi vijavyo iko taabani endapo viongozi wa leo watakosa kutimiza malengo yaliyowekwa.

Mwanasayansi  wa mazingira kutoka jijini Kisumu Bw Clifford Omondi, ameonya kuwa hali itazidi kudorora zaidi endapo mataifa tajiri yatakosa kuharakisha ukomeshaji wa matumizi ya kawi ya visukuku.

Bw Omondi pia ametoa changamoto kuhusu ahadi za fedha za kufidia waathirika wa mabadiliko ya tabianchi chini ya mpango wa ‘Loss and Damage Fund’ akidai huenda ukawa ahadi tupu za kufumba macho mataifa maskini na akataka mataifa tajiri kutimiza ahadi zao upesi.

“Hatutasalia na sayari hii tena endapo juhudi za kukomesha matumizi ya mafuta ya visukuku hazitapigiwa jeki,” Bw Omondi akasema.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Mpango wa Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kuhusu kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi (Climate Adaptation) iliyotangazwa katika COP28, ni kuwa mwaka wa 2022 ndiyo ulikuwa mwaka wa sita kuwa na joto zaidi juu ya viwango vilivyoripotiwa katika karne ya 20 na tangu mwaka wa 1880.

UAE hujulikana kwa sheria kali zinazozuia maandamano ya wafanyakazi, wanaharakati na hata maandamano ya kisiasa.

Kutumia hata mabango yoyote katika nchi hiyo, sharti watu au mashirika yapate idhini ya serikali.

Hofu ilitandaa kabla ya kongamano hilo huku wanaharakati wengi wa mabadiliko ya tabianchi wakihofia kuwa wangezuiliwa kufanya maandamano yao kuhusu mapengo mengi ambayo bado yapo kwenye vita dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wanaharakati wa mazingira wakiandamana jijini DUBAI katika Milki za Kiarabu (UAE). PICHA | JACOB WALTER

Mnamo Desemba 2, 2023, zaidi ya mataifa 117 yalitia saini mkataba wa kutaka kukomesha matumizi ya mafuta ya visukuku ifikapo mwaka wa 2050. Matifa hayo ni pamoja na Brazil, Nigeria, Australia, Japan, Canada, Chile, na Barbados.

Hata hivyo, mataifa ya China na India yalitoa tu kiashiria kuwa huenda yakakomesha matumizi ya mafuta hayo ifikapo mwaka wa 2030.

Kulingana na mkataba ulioafikiwa na viongozi wa kimataifa katika kongmano na COP28, mataifa yote yanatarajiwa kuungana katika kupunguza gesi ya kaboni kwa aslimia 43 ifikapo mwaka wa 2030.

  • Tags

You can share this post!

Raila na Kalonzo washauriwa wasitengane 

Wanachama wa UDA wanaokaidi Ruto kuadhibiwa

T L