• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Covid-19: Furaha China ikifungua mipaka yake

Covid-19: Furaha China ikifungua mipaka yake

NA MASHIRIKA

BEIJING, CHINA

CHINA hatimaye imeondoa vikwazo ilivyokuwa imeweka kuhusu usafiri wa nje ya nchi hiyo, hatua iliyomaliza masharti kwa watu wanaoingia katika taifa hilo kuwekwa kwenye karantini.

China imekuwa ikitekeleza masharti hayo kwa muda wa miaka mitatu.

Abiria wa kwanza waliwasili chini ya masharti hayo mapya katika viwanja vya ndege vya Guangzhou na Shenzhen, kusini mwa taifa hilo jana alfajiri, kulingana na Kituo cha Televisheni cha Serikali (CGTN).

Abiria hao 387 waliwasili kutoka Singapore na Canada. Hawakukaguliwa kuhusu ikiwa wameambukizwa virusi vya corona kama ilivyokuwa hapo awali. Pia, hawakuwekwa kwenye karantini kwa muda wa siku tano.

Hatua hiyo inafikisha mwisho masharti makali ambayo China imekuwa ikitekeleza dhidi ya watu wanaoingia nchini humo kutoka mataifa ya nje kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.

China ilianza kulegeza masharti hayo mwezi uliopita, kufuatia maandamano makali yaliyozuka dhidi ya serikali. Hata hivyo, hatua hiyo imekosolewa vikali, ikitajwa kuhatarisha maisha ya raia wake wapatao 1.4 bilioni kutokana wimbi jipya la maambukizi ambalo limeanza kushuhudiwa nchini humo. Hospitali nyingi zimelazimika kuchukua hatua mbadala kushughulikia idadi kubwa ya waathiriwa wa virusi hivyo wanaofika ili kutafuta matibabu.

Hatua hiyo pia inatoa nafasi kwa raia wengi kusafiri katika mataia ya nje kwa mara ya kwanza baada ya karibu miaka mitatu. Hili ni bila kuwa na hofu ya kuwekwa kwenye karantini baada ya kurejea nchini humo.

Licha ya hatua hiyo, taifa hilo halijawaruhusu watalii kuingia. Raia wa kigeni wanaruhusiwa tu kusafiri nchini humo kuwatembelea jamaa zao au kwa shughuli rasmi.

Wanahabari walisema jana kuwa raia wengi walifika barabarani kufurahia “mwisho halisi wa kutekelezwa kwa masharti makali ya corona”.

“Sababu ya kujitokeza kwetu ni kuwa hapo awali, ilikuwa vigumu kuondoka China bila kupitia taratibu nyingi za kubaini ikiwa umeambukizwa virusi vya corona au la. Watu wanahisi kama wamepata uhuru mpya kwenda kusafiri nje ya nchi,” akasema Katrina Yu.

Akaongeza: “Tovuti maarufu za usafiri zinaonyesha kuwa safari za ndege zimeongezeka kwa karibu asilimia 80 ikilinganishwa na muda kama huo mwaka 2022. Watu wengi wanataka kuelekea nchini Thailand. Wengine wanataka kusafiri mataifa kama Japan, Korea Kusini, Amerika na Australia.”

Hata hivyo, hatua hiyo imeyafanya mataifa kadhaa kuweka masharti makali kwa raia wanaosafiri huko kutoka China, yakihofia huenda wakaanza kuvisambaza.

Baadhi ya mataifa hayo ni Amerika, Japan, Canada, Uingereza, Ufaransa, Italia, Korea Kusini, Taiwan kati ya mengine.
Hata hivyo, China imekosoa masharti hayo kuwa “ya kibaguzi.”

Wataalamu wamesema hofu dhidi ya hatua ya China katika baadhi ya mataifa inaeleweka.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Ukame: Dua pekee si jibu bali teknolojia

AC Milan na AS Roma nguvu sawa katika Serie A huku Napoli...

T L