• Nairobi
  • Last Updated May 30th, 2023 1:21 PM
Israeli motoni kwa kuua mwanahabari

Israeli motoni kwa kuua mwanahabari

NA MASHIRIKA

RAMALLAH, PALESTINA

MWANAHABARI Shireen Abu Akleh wa shirika la habari la Al Jazeera, jana Alhamisi aliombolezwa kishujaa katika mji mkuu wa Palestina, Ramallah, baada ya kuuawa na vikosi vya Israeli Jumatano kwa kupigwa risasi.

Wapalestina walifanya ibada maalum kumkumbuka huku wakisisitiza kuwa wataelekea katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutafuta haki kufuatia mauaji yake.

Mwili wake uliondolewa Alhamisi asubuhi katika hospitali ya Istishari, eneo la West Bank na kupelekwa katika uwanja wa Ikulu ya Utawala wa Palestina.

Katika uwanja huo, Rais Mahmoud Abbas alimpa heshima zake za mwisho na kuuaga.Akihutubu kwenye ibada hiyo, Abbas alisisitiza kuwa Israeli ndiyo ilihusika kwenye mauaji hayo.

“Tunakataa Israeli kushiriki kwenye uchunguzi kuhusu mauaji ya Abu Akleh. Tutaenda katika ICC kutafuta haki,” akasema.

Ibada hiyo pia iliandamana na heshima za kijeshi katika uwanja huo.

Mwili huo baadaye ulipelekwa katika Hospitali ya St Louis French, eneo la Sheikh Jarrah, Jerusalem Mashariki, ambako familia yake huishi.

Mwanahabari huyo anazikwa leo Ijumaa katika eneo la Jerusalem Mashariki.

Wanahabari na waombolezaji walianza kukusanyika jana asubuhi katika hospitali hiyo kwa matayarisho ya hafla hiyo.

Jumatano, mwanahabari huyo, 51, aliombolezwa katika miji kadhaa ya Palestina kama Jenin, ambako aliuliwa.

Miji mingine ambako kuliandaliwa ibada maalum ni Neblus na Ramallah.Wapalestina pia walifanya maandamano ya amani katika miji kadhaa kulalamikia mauaji yake.

Walioshuhudia walisisitiza kuwa mwanahabari aliuawa na vikosi vya Israeli wakati alipokuwa akiangazia uvamizi uliokuwa umefanywa na vikosi hivyo mjini Jenin Jumatano.

Walikanusha madai ya awali ya Israeli kuwa wapiganaji wa Kipalestina ndio walihusika kwenye mauaji hayo.

Walisema kuwa mapigano yalikuwa yakiendelea katika eneo alimokuwa pamoja na wanahabari wengine, ambapo wote walikuwa na mavazi maalum kuwatambulisha kama wanahabari.

Kulingana na mwanahabari Ali al-Samoudi, ambaye pia anafanyia kazi shirika hilo, marehemu alipigwa risasi na vikosi vya Israeli.

Jana Alhamisi, Israeli ilionekana kubadili msimamo wake wa awali kukubali vikosi vyake vilihusika, baada ya maafisa wa ngazi za juu wa serikali kudai kuwa wapiganaji wa Kipalestina ndio walihusika.

Waziri Mkuu wa Israeli, Naftali Bennet, ni miongoni mwa maafisa ambao wamejitokeza kukanusha madai yanayovihusisha vikosi vyake na mauaji hayo.

Uchunguzi wa mwanzo hata hivyo umedhihirisha kuwa eneo ambako wanamgambo hao walinaswa kwa video wakifyatua risasi haliko mjini Jenin, kama ilivyodaiwa awali.

Mkuu wa jeshi la Israeli, Luteni Jenerali Aviv Kochavi, alisema kuwa haijabainika wazi aliyempiga risasi mwanahabari huyo.Marehemu alijiunga na shirika la Al Jazeera mwaka 1997, mwaka mmoja baada ya uzinduzi wake.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres, Alhamisi alieleza “kusikitishwa” na mauaji ya mwanahabari huyo.

Guterres aliomba idara husika kuchunguza mauaji hayo kwa kina na kuwachukulia hatua kali waliohusika.

“Ninakashifu vikali mashambulio yoyoye au mauaji yanayotekelezwa dhidi ya wanahabari. Kamwe, wanahabari hawapaswi kulengwa kwa vyovyote vile wakati wa vita,” akasema.

Nchini Amerika, Msemaji wa Ikulu ya White House, Jen Psaki, alisema kuwa Waamerika “wamesikitishwa vikali na mauaji ya mwandishi huyo.”

“Tunatoa risala za rambirambi kwa jamaa na marafiki wake,” akasema kupitia mtandao wa Twitter.

  • Tags

You can share this post!

Raila avuna lawama za dosari za Jubilee

Kioja hakimu akifanyia washtakiwa wa wizi harambee kortini

T L