• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 PM
Jina la Mackenzie lagonga mawakili kama radi kortini

Jina la Mackenzie lagonga mawakili kama radi kortini

Na RICHARD MUNGUTI

KUTAJWA kortini kwa jina la muhubiri Paul Mackenzie anayehusishwa na mauaji ya halaiki ya watu katika shamba la Shakahola katika kesi ya Pasta Ezekiel Odero kulipiga mioyo ya mawakili wake (Odero) kama radi.

Wakili Danstan Omari anayemtetea Odero katika kesi ya kufungwa kwa akaunti 30 za pasta huyo anayedai “hurudishia watu nyota zao zilizoibwa na Ibilisi” alinyanyuka kortini viongozi wa mashtaka James Gachoka na Virginia Kariuki kama mmoja aliyekanyaga kaa la moto huku akiwatahadharisha kamwe wasihusishe Odero na Mackenzie.”

Gachoka alisema mapasta hao wawili wanachunguzwa kwa ulanguzi wa pesa.

Polisi wanaamini mapasta hawa hupata mamilioni ya pesa kutoka mahala pasipo julikana.

“Kamwe usithubutu kuhusisha jina la Pasta Mackenzie na Kanisa la Pasta Ezekiel Odero. Pasta Mackenzie anahusishwa na mauaji ya halaiki ya watu katika mazingira tata Shakahola,” Omari aliwaonya viongozi wa mashtaka James Gachoka na Virginia Kariuki.

Wakili Omari aliwarukia Gachoka na Kariuki kwa kusema Pasta Odero anachunguzwa na polisi pamoja na Pasta Mackenzie kuhusu mauaji na maziko ya mamia ya watu katika shamba la Shakahola.

Kufikia sasa miili ya watu zaidi ya 200 imefukuliwa huku Pasta Mackenzi akizuiliwa gerezani kwa mauaji ya halaiki ya watu.

Polisi walipewa muda wa siku 90 kukamilisha uchunguzi.

Mtaalamu wa upasuaji wa Serikali Johansen Oduor amefanyia upasuaji maiti za waumini hao wa kanisa la Pasta Mackenzie.

Wakili Omari alitwangana na Gachoka kwa maneno na kusema “tuko kortini kuomba akaunti za Odero zifunguliwe.”

Aliongeza, “Serikali imekuwa ikiwala watoto na ndio maana imefunga akaunti za Odero anayewasaidia watoto zaidi ya 3,000.”

“Serikali haizai. Haifahamu uchungu wa kuzaa ndio maana imefunga akaunti za Odero ili watoto waangamie,” Omari alisema.

Pia aliifananisha serikali na mchawi anayeingia katika nyumba za watu usiku na kuroga.

“Polisi kama wachawi wameingia kortini na kufunga akaunti za Odero bila kujali madhara ya matendo yao,” alisema Omari.

Wakili huyo aliomba mahakama ifutilie mbali agizo la kufunga akaunti za Odero na kumruhusu atoe Sh50 milioni kufadhili mahitaji ya watoto.

  • Tags

You can share this post!

Dai wakristo wanateswa na serikali

Gesora Mwasi: Kuuza bidhaa mitandaoni kwahitaji ubunifu wa...

T L