• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Kenyatta: Ningali kiongozi wa Jubilee

Kenyatta: Ningali kiongozi wa Jubilee

NA SAMMY WAWERU

MVUTANO wa uongozi katika chama cha Jubilee unaendelea kutokota Rais mstaafu Uhuru Kenyatta akiwataka wapinzani wake kujua yeye ndiye angali kinara wa chama hicho.

Bw Kenyatta alisisitiza mnamo Jumatatu, Mei 22, 2023 kwamba hababaishwi na wanaotaka kumvua taji la uongozi chamani, akisema alivikwa kofia hiyo na wananchi.

Rais huyo wa tano wa Kenya alisema hivi: “Ningetaka wajue (wapinzani wake); Niliteuliwa na wananchi kuongoza chama, kisha wakanichague hadi nilipoachilia mamlaka na Wakenya ndio wataniondoa katika Jubilee.”

Alitoa matamshi hayo katika Kongamano la Kitaifa la Juibilee, mnamo Jumatatu, Mei 22, 2023 lililoandaliwa jijini Nairobi.

Majuzi, baadhi ya viongozi na wanasiasa wa Jubilee wanaoonekana kuegemea kwa serikali ya Kenya Kwanza walimbandua Kenyatta kutoka kwa wadhifa wake, nafasi yake ikitwaliwa na mbunge maalum Sabina Chege.

Katibu Mkuu wa chama hicho Bw Jeremiah Kioni, pia alivuliwa joho lake aliyekuwa mbunge wa Kieni Kanini Kega akitangazwa kumrithi.

Mabw Kenyatta na Kioni, hata hivyo, wakihutubu katika kongamano la Jubilee, walisisitiza kwamba wangali mamlakani.

Kwa upande wake rais huyo mstaafu, alionya wanaomchokoza akidai yeye hatishwi na yeyote.

“Wengine wanadhani siasa ni vitisho, nawaambia tafuteni mwingine ila si Uhuru wa Kenyatta. Kwa sababu Wakenya mliponipa uongozi wa chama na baadaye wa nchi, kulikuwa na muongozo mliotupa

Tulipomaliza, tulipeana uongozi kwa amani mchana hadharani,” alielezea.

Bw Kenyatta aidha aliwataka wapinzani wake kujua Jubilee ina wenyewe.

“Nawaambia waendelee, nawaambia chama kina wenyewe. Nimepewa niongoze hadi pale mtaniambia (wananchi) niache, nimkabidhi mwingine.”

Wandani wa Kenyatta wamekuwa wakinyooshea kidole cha lawama Dkt William Ruto, wakidai ndiye anachochea misukosuko chamani.

  • Tags

You can share this post!

Raila: Uhuru ni shujaa kwa kuhepa vitisho na kuandaa mkutano

Mbappe abeba PSG dhidi ya Auxerre

T L