• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 8:00 AM
Mackenzie aambia Kindiki anachopigana nacho kitamramba

Mackenzie aambia Kindiki anachopigana nacho kitamramba

NA BRIAN OCHARO

MSHUKIWA mkuu wa mauaji ya halaiki yaliyotokea Shakahola, Kaunti ya Kilifi, Paul Mackenzie, amemkashifu vikali Waziri wa Usalama, Prof Kithure Kindiki, aliyeapa kutumia kila njia kuhakikisha hataachiliwa huru.

Kupitia kwa wakili wake, Mackenzie na washukiwa wenzake 30 jana waliambia mahakama kwamba matamshi ya Prof Kindiki yanaashiria hawatatendewa haki.

Wakili Wycliffe Makasembo, alidai kuwa wateja wake sasa wamesusia kula wakilalamikia matamshi ya waziri huyo wakisema yanatishia haki yao ya kikatiba kuhesabiwa kuwa hawana hatia hadi itakapothibitishwa vinginevyo.

“Baadhi ya washukiwa wamegoma kula. Maneno ambayo yalisemwa na Prof Kindiki ni hatari, ni kinyume cha sheria na hayastahili kabisa,” Bw Makasembo alimweleza Hakimu Mwandamizi Mkuu wa Shanzu, Bw Yusuf Shikanda.

Pia, wametishia kususia kesi iwapo Prof Kindiki hatabatilisha matamshi yake.

“Tunahitaji hakikisho kutoka kwa Jaji Mkuu Martha Koome, Idara ya Upelelezi wa Jinai na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili (LSK) kuwa washukiwa watapata haki,” akasema wakili huyo.

Hata hivyo, Kiongozi wa Mashtaka, Ogega Bosibori, aliomba korti kupuuza malalamishi hayo akisema yameletwa katika jukwaa lisilofaa.

Hakimu alisema hakuna jinsi matamshi yanayoenezwa nje ya mahakama yanaweza kushawishi maamuzi yatakayotolewa.

“Prof Kindiki ni afisa wa ngazi za juu serikalini, na kwa mwananchi wa kawaida, matamshi yake yanaweza kuwa na uzito zaidi. Hata hivyo, ninawahakikishia washukiwa kwamba mahakama hii itasimamia haki,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Rais Samia Suluhu akatizia Wakenya ugali mpakani

Shule moja nchini Nigeria yawaruhusu wazazi kulipa karo kwa...

T L