• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 10:30 AM
Milio ya risasi kutulia kwa muda katika Ukanda wa Gaza

Milio ya risasi kutulia kwa muda katika Ukanda wa Gaza

NA MASHIRIKA

JERUSALEM, ISRAELI

PANDE hasimu za Israeli na kundi la Hamas zimekubali kurefusha muda wa kusitisha mapigano kwa siku mbili zaidi.

Tangazo hilo ni afueni kwa waathiriwa wa mapigano hayo.

Kulingana na maafisa wa Qatar, makubaliano hayo yatakuwa ya siku mbili na kuna matumaini yatajumuisha kuachiliwa huru kwa mateka wa Israeli waliokamatwa na kundi la Hamas.

Msemaji wa wizara ya mambo ya Kigeni wa Qatar ni miongoni mwa maafisa walioeleza habari hizo kupitia mtandao wa kijamii wa X.

Katika makubaliano ya hapo awali ambapo mapigano hayo yalisitishwaa kwa siku nne, kundi la Hamas lilikuwa likiwaachia mateka kadhaa wa Israeli kila siku.

Hata hivyo, Israeli bado inasubiri idhini ya serikali yake kabla ya makubaliano yaliyotangazwa jana kuanza kutumika.

Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, ameiomba serikali yake ikubali kurefusha mkataba wa kusitisha operesheni zake katika Ukanda wa Gaza ili mateka zaidi waachiliwe.

Maafisa wa Qatar ambao wanashirikiana na Amerika kuratibu mashauriano kati ya Israeli na kundi la Hamas wamesema wana imani kubwa kwamba usitishaji mapigano kwa siku mbili zaidi utaidhinishwa nchini Israeli.

Netanyahu alisema Rais wa Amerika, Joe Biden amesaidia sana kufanikisha makubaliano hayo ya sasa yatakayowezesha kuachiwa mateka zaidi bila upande wa Israeli kutimiza matakwa mengi ya kundi la Hamas.

Hata hivyo, amesisitiza kwamba malengo ya Israeli kwenye vita vyake dhidi ya Hamas hayajabadilika.

“Kuhusiana na suala la mateka, tunaendelea kutekeleza tulichokubaliana na pia tunaendelea na lengo letu kuu tulilolitaja – kuhakikisha mateka wetu wanarejea nyumbani, kulitokomeza kabisa kundi la Hamas, na bila shaka kuhakikisha kwamba tukio kama hilo halijitokezi tena,” akasema Netanyahu.

Tangu awamu ya kwanza ya usitishaji mapigano ilipoanza Ijumaa iliyopita, jumla ya mateka 69 wameachiwa huru na kundi la Hamas huku Israeli ikiwaachilia huru wafunga 150 wa Kipalestina na msaada mkubwa wa kibinadamu kuruhusiwa kuingia Ukanda wa Gaza.

Inaaminika zaidi ya mateka 200 walichukuliwa na kundi la Hamas. Hapo jana wengine zaidi waliachiwa huru ikiwemo vijana wawili raia wa Ujerumani.

Hadi sasa mamlaka za Ukanda wa Gaza zinasema watu wapatao 14,000 wameuawa tangu Israeli ilipoanza kufanya mashambulizi yake ya kulipiza kisasi.

Wakati uo huo, Waziri wa Mambo ya Nje Amerika, Antony Blinken, anatarajiwa kufanya ziara nyingine Mashariki ya Kati wiki hii ikiwa ni ya tatu tangu mapigano kuzuka Ukanda wa Gaza.

Hayo yalielezwa na ofisi yake Jumatatu.

Blinken anatarajiwa kukutana na Netanyahu na rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mamhoud Abbas mjini Ramallah.

Ananuia kupigia debe usambazaji wa misaada ya kibinadamu kwenye Ukanda wa Gaza na kuachiliwa kwa mateka wote.

  • Tags

You can share this post!

Si kila mwasho ukeni husababishwa na kuambukizwa magonjwa...

Shabiki sugu wa Gor na Arsenal ashinda Sh27 milioni za...

T L