• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Mkenya wa miaka 52 ashtakiwa Amerika kwa kupanga kuua bibi yake 

Mkenya wa miaka 52 ashtakiwa Amerika kwa kupanga kuua bibi yake 

NA MWANGI MUIRURI 

MWANAMUME Mkenya ameshtakiwa nchini Amerika kwa makosa ya kujaribu kupanga njama kuua mwanamke wa familia yao.

Bw Leonald Thuo Mwithaga, mwenye umri wa miaka 52 ameshtakiwa kwamba alijaribu kufadhili njama hiyo nchini Amerika.

Stakabadhi ambazo zimewasilishwa mahakamani ambapo ameachiliwa kwa bodi ya Dola 5 milioni za Amerika (Sh766.5 milioni) zinadai kwamba alijaribu kumshawishi dereva wa teksi kumsaidia kupata muuaji wa kutekeleza mauti hayo.

Bw Mwithaga alishtakiwa rasmi Desemba 5, 2023 baada ya kukamatwa Desemba 4, 2023.

Dereva wa teksi ndiye alifika katika kituo cha polisi na kuripoti kwamba Bw Mwithaga alikuwa amejaribu kumsajili katika njama hiyo ya mauaji.

“Bw Mwithaga ambaye alikuwa akifanya kazi nchini humo kama meneja wa benki alikuwa amepanga mauaji hayo yatekelezwe kati ya Januari 28, 2024 na Februari 3, 2024 kwa kuwa angekuwa amesafiri hadi nchini Kenya basi kumwondolea hatari ya kuwa mshukiwa,” taarifa ya mashtaka inasema.

Baada ya kuacha kazi Juni 2023, alipania kurudi nchini Kenya Desemba 7, 2023.

Bw Mwithaga anasemwa kwamba alikuwa katika maandalizi ya kutekeleza mauaji hayo na ambapo kati ya Septemba 9 na Desemba 1, 2023 alikuwa akizidisha njama hiyo kupitia kusaka muuaji wa kulipwa.

Tarehe ambazo zimetiliwa mkazo katika mashtaka hayo ni Oktoba 26, 2023 ambapo Bw Mwithaga anadaiwa kutumia maneno kwamba “nataka muuaji ambaye anaweza kuweka huyo mwanamke chini”.

Novemba 3, 2023 anadaiwa kwamba alisema “natamani sana mtu wa kugonga mwanamke huyu na ammalize”.

Nayo Desemba 1, 2023 Mwithaga anadaiwa kwamba alitaka mwanamke huyo “adungwe na sumu ambayo itamsababishia maradhi makuu sawa na Kansa”.

Baada ya dereva huyo wa teksi kupiga ripoti kuhusu njama ya Bw Mwithaga, stakabadhi za mashtaka zinaeleza, mpelelezi wa polisi alijitokeza akijitambulisha kama muuaji ambaye angempeleka mlengwa kwa hepi na amuwekee sumu kwa mapochopocho ya sherehe.

Ni baada ya Bw Mwithaga kujadiliana na afisa huyo kuhusu njama hiyo ya mauaji bila kujua alikuwa akijiingiza kikangaoni ambapo alitiwa mbaroni na akashtakiwa kwa madai ya ujambazi wa kupanga mauaji na pia kutishia maisha ya shahidi.

Kwa sasa, Bw Mwithiga ameamrishwa kurejesha kwa serikali ya Amerika na bunduki zote alizokuwa amesajiliwa kumiliki, huku akionywa kubakia umbali wa futi 2, 500 kutoka kwa shahidi wote katika mashtaka hayo yanayomkabili.

Aidha, pasipoti yake imetwaliwa na hawezi akatoka Mji wa Connecticut na kwa wakati wote atakuwa chini ya ujasusi wa kiteknolojia kwa masaa 24 hadi kesi yake iamuliwe.

Atarejea kortini mnamo Januari 26, 2024.

 

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mshukiwa wa ulghai alivyotiririkwa na machozi akililia...

Walanguzi wa dawa za kulevya wasukumwa jela kula maharagwe

T L