• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:39 PM
Museveni asaini mswada ambao unapinga ushoga

Museveni asaini mswada ambao unapinga ushoga

NA DAILY MONITOR

KAMPALA, UGANDA

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda jana alitia saini mswada tata unaopinga ushoga na unaopendekeza vifungo vya maisha kwa wale watakaopatikana wakijihusisha katika vitendo hivyo.

Rais Museveni alitia saini mswada huo baada ya kufanyiwa mabadiliko, ili kuweka masharti makali kwa wale wanaojihusisha na vitendo hivyo.

“Rais Museveni ametekeleza jukumu lake la kikatiba kama ilivyo kwenye Kipengele 91 (3) (a) cha Katiba ya 1995 na kutia saini Mswada wa Kupinga Ushoga, 2023,” akasema Jumatatu, Anita Among, ambaye ndiye Spika wa Bunge la taifa hilo.

“Tumesimama kidete kutetea utamaduni, maadili na matamanio ya watu wetu kulingana na malengo 19 na 24 kitaifa na sera ya taifa letu,” akaongeza. Rais Museveni alitia saini mswada huo tata licha ya ukosoaji mkali ambao amekuwa akipata kutoka kwa mataifa ya Magharibi na wanaharakati wa haki za binadamu.

Mswada huo ulipitishwa mara ya kwanza na wabunge mnamo Machi, lakini ulirejeshwa Bungeni ili kufanyiwa mageuzi. Kulingana na mswada huo mpya, mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kushiriki ngono na mtu wa jinsia yake atachukuliwa kuwa shoga. Chini ya mswada huo, watu hao watakabiliwa na kifungo cha maisha.

Mswada huo pia unapendekeza kifungo cha maisha kwa dhuluma za ngono dhidi ya watoto, walemavu au katika hali ambapo mwathiriwa wa kitendo cha ngono ameambukizwa maradhi hatari.

Raia pia watahitajika kuripoti kwa idara za serikali vitendo vyovyote vya dhuluma za kimapenzi dhidi ya watoto wao na watu wengine katika jamii. Hapo awali, sheria hiyo ilitaja kujitambulisha kama shoga hadharani kuwa kosa, ijapokuwa Museveni akasema kuwa hilo lingesababisha watu wasio na hatia kukamatwa kutokana na mwonekano wao tu. Kipengele hicho kiliondolewa baada yake kuurejesha katika Bunge.

Licha ya mswada huo kuidhinishwa kuwa sheria, baadhi ya wadadisi wanasema kuna uwezekano baadhi ya mapendekezo yake yatawasilishwa mahakamani. Sheria kama hiyo ilifutuliwa mbali na Mahakama ya Kikatiba ya Uganda mnamo 2014. Hapo jana, alisema Among kupitia mtandao wa Twitter: “Ninawarai wahusika sasa kutekeleza sheria hiyo kikamilifu.” “Raia wa Uganda wamezungumza.

Ni wajibu wenu kuhakikisha sheria hiyo imezingatiwa kabisa,” akaongeza. Awali, wanaharakati walifika mahakamani kupinga kujadiliwa na kupitishwa kwa mswada huo, wakirejelea baadhi ya mapendekezo makali dhidi ya wale watakaopatikana na hatia. Wadadisi wanasema kuwa hatua ya Rais Museveni itafungua ukurasa mpya wa mvutano baina yake na mataifa ya Magharibi.

Baadhi ya nchi hizo kama Amerika zimetishia kusimamisha utoaji misaada ya kifedha kwa taifa hilo, ikiwa litaendelea “kuhujumu haki za mashoga kupitia utekelezaji wa mswada huo tata”.

  • Tags

You can share this post!

Maina Njenga aachiliwa kwa dhamana wakili wake akidai...

Raila atabasamu korti ikizaba Ruto

T L