• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
Raila: Uhuru ni shujaa kwa kuhepa vitisho na kuandaa mkutano

Raila: Uhuru ni shujaa kwa kuhepa vitisho na kuandaa mkutano

Na WANGU KANURI

KINARA wa upinzani, Raila Odinga amemshukuru aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kwa kusimama imara na kuhepa vitisho vyote vilivyogomea chama chake cha Jubilee.

Bw Odinga ambaye amekuwa akikiuka sheria na kufanya maandamano alisema kuwa ndugu yake Bw Kenyatta alihepa vitisho vya kusema chama cha Jubilee hakitafanya mkutano mnamo Jumatatu, Mei 22, 2023.

“Hayawi hayawi huwa…walisema haitawezekana lakini WanaJubilee na WanaAzimio wakawajibu itawezekana. Natoa shukrani kwa ndugu yangu Uhuru Kenyatta kwa kusimama imara na kuhepa vitisho vyote vya kusema chama cha Jubilee hakitafanya mkutano siku ya leo,” akasema.

Isitoshe, Bw Odinga aliwasuta wanaotaka kuchukua usukani wa chama cha Jubilee na kukipatia viongozi wa Kenya Kwanza huku akisema kuwa wataangamia kwenye mipango yao.

Akiongeza kuwa viongozi hao hawajui wanachojihusisha nacho na kitaondokea kuwaramba, Bw Odinga aliwaeleza kuwa mwishowe watakuja kujutia matendo yao.

Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Ngong Racecourse uliitishwa na Bw Kenyatta katika juhudi za kurejesha utulivu katika chama alichotumia kutawala.

Mgogoro unaoshuhudiwa kwenye chama hicho unazingira uongozi na umejitawanya kwa makundi mawili.

Kundi moja linaongozwa na Jeremiah Kioni anayeungwa mkono na Bw Kenyatta na linguine linaongozwa na mbunge maalum Sabina Chege na mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki  (EALA), Kanini Kega.

Bi Chege alikuwa ametwikwa wadhifa wa kaimu kiongozi wa chama na mrengo wake ukajitenga na mkutano ulioitishwa na Bw Kenyatta jaribio ambalo mrengo wa Bw Kioni umepuuza.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Jubilee David Murathe alisema kuwa mkutano huo maalumu wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) utafanywa Jumatatu na Jumanne 23, 2023.

Barua ya Bomas kwa chama hicho ilizua wasiwasi wa kutofanyika kwa mkutano huo baada ya usimamizi wa Bomas ulisema kuwa ukumbi waliotaka kufanyia mkutano wao hautapatikana.

Bw Murathe alijibu kwa kusema kuwa chama hicho kitatafuta ukumbi mwingine wa kufanyia mkutano kabla ya Jumatatu.

  • Tags

You can share this post!

Karua amshambulia Ruto kuhusu ushuru

Kenyatta: Ningali kiongozi wa Jubilee

T L