• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
Rais Biden aanguka baada ya kuongoza hafla ya kufuzu kwa wanajeshi

Rais Biden aanguka baada ya kuongoza hafla ya kufuzu kwa wanajeshi

Na MASHIRIKA

RAIS wa Amerika Joe Biden mnamo Alhamisi alijikwaa na kuanguka baada ya kuongoza hafla ya kufuzu kwa wanajeshi katika Chuo cha Mafunzo ya Kikosi cha Wanajeshi wa Angani mjini Colorado, Amerika.

Wanajeshi na walinzi wake walichukua hatua za haraka kumsaidia na kumnyanyua Rais huyo mwenye umri wa miaka 80.

Hata hivyo, aliwahakikishia walinzi wake kwamba hakuumia huku akiwaonyesha kifaa ambacho kilimtega.

Baadaye alitembea bila kusaidiwa hadi kwa kiti chake huku akitabasamu.

Awali, Rais Biden alikuwa amewahutubia maafisa wa kijeshi wa cheo cha Cadet waliofuzu kwa shahada za diploma baada ya kupokea mafunzo katika chuo hicho.

Alitumia muda wa dakika 90 akipeana vyeti vya kufuzu na kuwapongeza mamia ya wanajeshi.

“Rais yuko sawa. Kifaa cha kushikilia kipaza sauti ndicho kilimtega alipokuwa akiondoka jukwaani,” msemaji wa Ikulu ya White House Ben LaBolt akaandika katika mtandao wa Twitter.

Rais Biden hakujibu maswali kutoka kwa wanahabari baada ya kisa hicho na aliondoka Colorado saa moja baada ya tukio hilo.

Hii sio mara ya kwanza kwa rais huyo kuanguka hadharani. Kwa mfano, mwaka 2022 alianguka alipokuwa akiendesha baiskeli mjini Delaware. Pia amewahi kuonekana akiteleza na kuanguka kwenye ngazi akiabiri ndege rasmi ya rais wa Amerika, maarufu kama Airforce One.

Licha ya visa hivyo, madaktari wa Rais Biden wanasema ni buheri wa afya na anaweza kuendelea kutekeleza majukumu yake.

Kiongozi huyo ametangaza kuwa atatetea kiti chake katika uchaguzi wa urais utakaofanyika mnamo Novemba 2024.

TAFSIRI: CHARLES WASONGA

  • Tags

You can share this post!

Jenerali Ogolla achapa kibarua cha kwanza katika Sherehe ya...

MKU yakariri kujitolea kuendelea kushiriki makongamano ya...

T L