• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Seneta Onyonka: Rais Ruto yafanye magazeti kuwa rafiki utajua mahangaiko ya Wakenya   

Seneta Onyonka: Rais Ruto yafanye magazeti kuwa rafiki utajua mahangaiko ya Wakenya  

 

NA SAMMY WAWERU

SENETA wa Kisii Richard Onyonka amejiunga na kundi la viongozi wa kisiasa wanaopinga kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2023.

Mswada huo wa serikali ya Kenya Kwanza, unapendekeza nyongeza ya ushuru (VAT) wa mafuta ya petroli kutoka asilimia ya sasa 8 hadi 16 Bw Onyonka akisema ongezeko hilo litachangia gharama ya maisha kuongezeka mara dufu.

Wananchi wanateseka licha ya ahadi chungu nzima za Rais William Ruto wakati akiomba kura 2022, mswada huo hauhitajiki kwa sasa, alisema seneta huyo wa Kaunti ya Kisii.

Alisema badala yake, Dkt Ruto anapaswa kuwa rafiki wa magazeti na vyombo vya habari kujua Wakenya wanavyohangaika.

Mswada huo vilevile unapendekeza kukatwa kwa asilimia 3 ya mshahara wa watu walioajiriwa ili kufanikisha mpango wa nyumba za bei nafuu.

“Tafadhali Mheshimiwa Rais soma magazeti, wananchi wamekataa mambo ya nyumba za bei nafuu,” Bw Nyonka alisema.

Mwanasiasa huyo alisema Rais Ruto anapaswa kuleta mjadala wa jinsi gharama ya maisha itapunguzwa, kama alivyoahidi wakati wa kampeni 2022 akiwa naibu wa rais.

“Punguza bei ya bidhaa za kimsingi; unga, sukari, na mafuta, miongoni mwa zingine,” alishauri.

Endapo Mswada wa Fedha 2023 utapitishwa na bunge, gharama ya maisha na uchumi inatarajiwa kuongezeka maradufu.

Tayari bei ya unga, sukari na mafuta ya kupika imeanza kuongezeka.

“Kuanzia Juni 2023, bei ya mafuta itakuwa ghali. Maisha yataenda juu mara dufu,” alionya seneta Onyonka.

Mwanasiasa huyo wa mrengo wa upinzani, amejiunga na viongozi na vinara wenza kupinga mswada huo.

Kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga aliye pia kiongozi wa ODM ametangaza kwamba atashawishi wabunge wake kuangusha mswada huo.

  • Tags

You can share this post!

Messi aweka rekodi mpya ya ufungaji mabao bara Ulaya

Kioja ndume wa kupigana wakifurusha waombolezaji Kakamega ...

T L