• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 5:55 PM
Sokomoko mpya Amerika raia mwingine mweusi akiuawa

Sokomoko mpya Amerika raia mwingine mweusi akiuawa

NA MASHIRIKA

MAANDAMANO makubwa jana yalizuka viungani mwa jiji la Mineapolis, Amerika baada ya polisi kumpiga risasi raia mweusi karibu na mahali ambapo George Floyd aliuawa mwaka uliopita.

Kulingana na mwanahabari mmoja aliyenasa tukio hilo kwa video, polisi walilazimika kufyatua risasi hewani kutibua maandamano hayo ambayo yametonesha kidonda cha mauaji ya Floyd. Kesi ya Floyd bado inaendelea huku afisa aliyemuua bado akikabiliwa na mashtaka ya mauaji kortini.

Mamake mwanaume huyo kwa jina Daunte Wright ambaye alikuwa na umri wa miaka 20 pekee, aliwasimulia wanahabari kuwa mwanawe alikuwa amempigia simu akisema alikuwa anabururwa na polisi.

Kate Wright alisema aliwasikia polisi wakimwaagiza mwanawe aweke simu yake chini kisha wakakatiza mawasiliano kati yao. Baada ya muda mchache mpenzi wa mwanawe alimwaarifu kuwa alikuwa amepigwa risasi na polisi garini.

Idara ya kupeleleza visa vya uhalifu Minnesota ilithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na ikafichua kuwa inamchunguza afisa aliyetekeleza mauaji hayo japo haikufichua jina lake.

Kulingana na taarifa kutoka kituo cha polisi cha Brooklyn, maafisa wa usalama walimtoa dereva (marehemu) kutoka kwa gari lake kwa kukiuka sheria za trafiki. Walibaini kuwa alikuwa ana hati ya kukamatwa kwa makosa ya awali na wakaamua apelekwa kizuizini.

Hata hivyo, dereva huyo alirejea katika gari lake na mmoja wa afisa wa polisi akampiga risasi ndipo akafa papo hapo. Taarifa hiyo iliongeza kwamba, mwanamke aliyekuwa kwenye gari hilo pia alipata majeraha madogo na akakimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Kutokana na kisa hicho, waandamanaji waliojazana barabarani waliwasha mishumaa na kubeba mabango yenye maandishi ‘Haki kwa Daunte Wright’. Baadhi walivunja vyoo vya magari ya polisi huku makabiliano yakichacha.

Meya wa Brooklyn Mike Elliot alitaja mauaji ya Wright kama ya kusikitisha na akawaomba waandamanaji wawe watulivu uchunguzi ukiendelea.

“Tunawaomba waandamanaji wadumishe amani na polisi nao pia wajizuie kutumia nguvu kupita kiasi kuwakabili,” akaandika Elliot kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mauaji hayo yanajiri wakati aliyekuwa afisa wa polisi, Dereck Chauvin anakabiliwa na kesi ya mauaji ya Floyd mnamo Mei mwaka jana.

Mauaji ya Floyd kama tu ya Wright yalizua maandamano makali Amerika huku raia wakikemea ubaguzi wa rangi na dhuluma zinazotekelezwa na polisi dhidi ya raia weusi.

You can share this post!

Uganda kuanza kuuza mafuta 2025

UCL: Bayern na PSG kukabana tena