• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:20 PM
Trump aacha Amerika yenye aibu na ubaguzi

Trump aacha Amerika yenye aibu na ubaguzi

Na AFP

JOE Biden ataapishwa saa chache kutoka sasa kuwa rais wa 46 wa Amerika kwenye sherehe ambayo Rais Donald Trump amesema atasusia.

Maelfu ya maafisa wa usalama wakiwemo wanajeshi wamemwagwa jijini Washington, ambako sherehe ya uapisho itafanyika, kwa ajili ya kulinda usalama kufuatia kisa cha Januari 6 mwaka huu ambapo wafuasi wa Trump walifanya jaribio la kupindua serikali, na kuacha watu watano wakiwa wamekufa.

Kuapishwa kwa Biden kutafungua ukurasa mpya baada ya kipindi cha miaka minne kilichokumbwa na matatizo na migawanyiko tele chini ya utawala wa Trump.

Biden, ambaye alihudumu akiwa seneta wa chama cha Democratic kwa miaka mingi na pia alikuwa makamu wa rais wa Barack Obama, jana alielekea Washington akiandamana na mkewe Jill Biden kutoka nyumbani kwao jimbo la Delaware.

Biden ataapishwa pamoja na makamu rais mpya Kamala Harris, ambaye ni mwanamke wa kwanza kuwahi kushikilia afisi hiyo.

Kwa upande wake, Trump alitumia siku yake ya mwisho jana katika Ikulu ya White House akishughulikia orodha ndefu ya watu waliosubiri msamaha wa urais kabla ya kususia hafla ya kumwapisha mrithi wake na kuelekea Florida.

Kulingana na vyombo vya habari Amerika, orodha hiyo ilijumuisha wahalifu wapatao 100.

Kundi hilo lilijumuisha wahalifu wa kitaaluma na watu ambao kesi zao zimepigiwa debe na wanaharakati wa haki kwa wahalifu katika kile kinachotajwa na ripoti nchini humo kama juhudi kali za ushawishi.

Trump amekuwa kimya katika siku za hivi karibuni ambayo si kawaida yake huku akijitayarisha kuanza maisha mapya katika makao yake ya Mar-a-Lago Golf Club, Palm Beach.Baada ya kupigwa marufuku na mtandao wa kijamii wa Twitter kwa kuchapisha jumbe nyingi za kupotosha, amekatiza pakubwa kuwasiliana na taifa.

Kufikia jana Trump hakuwa amempongeza Biden wala kumwalika kwa kikombe cha chai katika Afisi ya Oval kuambatana na utamaduni kabla ya uapishaji wa rais nchini humo.

Badala yake, Trump amekuwa akitumia muda wake kukutana na kundi linalozidi kudidimia la wafuasi wake wa dhati waliomuunga mkono wakati wa juhudi za miezi miwili zilizogonga mwamba za kupindua matokeo ya uchaguzi wa Novemba.

Juhudi hizo zilifikia kilele mnamo Januari 6 huku Trump akihimiza umati wa watu kuandamana hadi Congress.Baada ya umma kuwalemea polisi, kumuua afisa mmoja na kuvuruga jumba la Capitol, Trump alitimuliwa kwa mara ya pili, kisa kingine cha kwanza kabisa kuwahi kutokea katika urais.

You can share this post!

Msimu wa utapeli waanza

Bobi Wine alia njaa majeshi yekiendelea kumfungia nyumbani...