• Nairobi
  • Last Updated June 1st, 2023 12:23 AM
Ugaidi: 6 wafa, 33 wakiumia Uganda

Ugaidi: 6 wafa, 33 wakiumia Uganda

Na FRANLIN DRAKU, Mwandishi wa NMG, Kampala, Uganda

POLISI nchini Uganda jana Jumanne walithibitisha kuwa milipuko miwili iliyotokea jijini Kampala ilitekelezwa na washambuliaji watatu wa kujitoa mhanga ambao walifariki papo hapo.

Milipuko hiyo ilitokea katika kizuizi kimoja cha polisi, na barabara ya Parliament Avenue, karibu na majengo ya bunge, katikati ya jiji hilo.

Idara ya Polisi ilisema kuwa raia wengine watatu walifariki na wengine 33 wakajeruhiwa, ingawa huenda idadi ya waliofariki ikawa juu zaidi ya iliyoripotiwa kufikia jana Jumanne usiku.

Watano kati ya waliojeruhiwa wako katika hali mbaya, kulingana na msemaji wa polisi, kamishna Fred EnangaBw Enanga aliwaambia wanahabari kwamba shambulio dhidi ya polisi lilitekelezwa na mmoja wa washambuliaji hao aliyenaswa kwenye kamera ya CCTV akibeba begi mgongoni kabla ya kuilipua.

Raia wawili walifariki papo hapo na wengine 17 wakajeruhiwa na kukimbizwa hospitalini.Shambulio katika barabara ya Parliament Avenue lilitekelezwa na washambuliaji wawili waliokuwa wakisafiri kwa bodaboda.

Raia mmoja aliuawa katika mlipuko huo uliotokea karibu na majumba ya Raj Chambers na Jubilee Insurance.

Polisi walisema mshambuliaji wa nne alifukuzwa na kukamatwa katika eneo la Bwaise kitongoji cha Kampala baada ya kupigwa risasi na kulemazwa na maafisa wa polisi.

Milipuko hiyo iliyotokea dakika tatu baada ya jingine – kati ya saa nne na dakika 3 na saa nne na dakika 6 – ilitekelezwa na magaidi wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na kundi la Allied Democrativ Forces (ADF).

Walitumia vilipuzi vya kujitengenezea (IEDs), kulingana na duru za polisi.Bunge la Uganda lilisitisha shughuli zake, kwa muda kufuatia matukio hayo ambayo yalisababisha taharuki kubwa jijini Kampala na taifa hilo kwa ujumla.

Naibu Spika wa bunge hilo Anita Among aliwaagiza wabunge kusalia nyumbani kwa muda usiojulikana ili kutoa nafasi kwa uchunguzi.

“Bunge limefungwa na wabunge wanashauriwa kutofika hapa, ila wasalie nyumbani,” Bi Among akasema.

Naibu huyo wa Spika alifafanua kuwa shughuli zote za bunge hilo zilisitishwa ikiwemo mikutano ya kamati zake; ya ana kwa ana au kupitia mitandaoni.

Maafisa wa polisi pia waliziba barabara zote za kuingia na kuondoka katikati mwa jiji la Kampala.

Picha zilizosambazwa mitandaoni zilionyesha magari yakiteketea.

Hii ni mara ya tatu ndani ya muda wa miezi miwili kwa milipuko ya mabomu kutokea nchini Uganda.

Oktoba, watu wawili waliuawa na wengine kadha wakajeruhiwa katika mlipuko uliotokea katika mkahawa moja maarufu viungani mwa jiji la Kampala.

Ulitokea ndani ya mkahawa kwa jina Digida Eating Point ulioko eneo la Komamboga.

“Eneo la tukio limezingirwa na maafisa wa usalama kutoka kitengo cha kuchunguza mabomu wameitwa kuchunguza ikiwa mlipuko huo ni wa kimakusudi au la. Tunawashauri wananchi kuwa watulivu huku tukichunguza chanzo cha tukio hili,” msemaji wa polisi Fred Enanga akasema kupitia taarifa.

Mlipuko huo ulijiri baada ya mashirika kadha ya habari kuripoti kwamba Uingereza ilionya raia wake kuwa wafuasi wa kundi moja la kigaidi walikuwa wakipanga kushambulia Uganda.

Jumla ya watu 74 waliuawa katika shambulio la bomu lililotekelezwa na magaidi jijini Kampala mnamo Juni 12, 2010.

Watu hao walikuwa miongoni mwa mamia ya mashabiki wa kandanda waliokuwa wakitizama mechi ya fainali ya Kombe la Dunia ndani ya klabu moja katikati mwa jiji hilo.

Milipuko ya Jumanne imetokea siku chache kabla ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni kuongoza mkutano wa marais wa mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki kujadili mapigano yanayoendelea nchini Ethiopia.

Rais Uhuru Kenyatta ni miongoni mwa viongozi walioalikwa katika mkutano huo ambao ulikuwa umeratibiwa kufanyika jijini Kampala.

Haikujulikana ikiwa mkutano huo bado utaendelea ulivyopangwa.

Mchakato wa kurejesha utulivu nchini Ethiopia ulishika kasi Alhamisi wiki jana baada ya mjumbe maalum wa Amerika anayesimamia Upembe mwa Afrika Jeffrey Feltman kuwasili nchini humo.

Rais Kenyatta pia alizuru taifa hilo ambapo alifanya mashauriano ya kina na Waziri Mkuu Abiy Ahmed.

You can share this post!

Ukiukaji wa haki za Miguna hatari kwa nchi – Mutunga

ZARAA: Wakulima wapiga mabroka chenga

T L