• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 10:30 AM
Waliohusika na sheria dhidi ya ushoga Uganda kunyimwa kibali cha kuingia Amerika

Waliohusika na sheria dhidi ya ushoga Uganda kunyimwa kibali cha kuingia Amerika

NA MASHIRIKA

KAMPALA, UGANDA

AMERIKA ilidokeza Jumatatu kuwa itafutilia mbali viza za maafisa wa Uganda ambao walihusika na sheria tata dhidi ya mashoga.

Waziri wa Mambo ya Nje, Antony Blinken, alisema kuwa Amerika itawazuia maafisa wa sasa au wa zamani, na familia zao kuzuru nchi yao ikiwa watapatikana kuhusika na sheria tata dhidi ya mashoga.

“Makundi hayo yanajumuisha, lakini sio tu, wanaharakati wa mazingira, watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari, watu wa LGBTQI+ na waandamanaji wa mashirika ya kiraia,” Blinken alisema katika taarifa.

“Kwa mara nyingine tena ninaihimiza sana serikali ya Uganda kufanya juhudi za pamoja za kutetea demokrasia na kuheshimu na kulinda haki za binadamu ili tuweze kudumisha ushirikiano wa miongo kadhaa kati ya nchi zetu ambao umewanufaisha Wamarekani na Waganda pia,” alisema.

Rais wa Amerika, Joe Biden, Umoja wa Ulaya na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, wamekuwa wakiikosoa vikali Uganda kufuatia sheria kali dhidi ya ushoga.

Hata hivyo, Rais Yoweri Museveni, ameapa kupinga shinikizo la kimataifa kuhusu sheria hiyo, ambayo inaungwa mkono na nchi nyingi.

Mnamo Mei, Amerika ilifutilia mbali viza ya spika wa bunge la kitaifa wa Uganda Anita Among baada ya kupitisha sheria za kutotambua mashoga na wasagaji nchini humo.

Kulingana Asuman Basalirwa, aliyewasilisha mswada huo, ujumbe huo wa kufutilia mbali viza ya spika huyo, ulithibitishwa kupitia barua pepe.

Akinukuu ujumbe huo baada Rais Museveni, kupuuzilia mbali shinikizo kutoka kwa mataifa ya magharibi na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu kutaka kuunga mkono mswada kupinga ushoga kuwa sheria.

“Taifa la Amerika limetupilia mbali viza ya spika wa Uganda. Kwa sasa Anita Among hana viza ya Anerika,” alisema huku akionyesha nakala ya barua pepe hiyo kwa wanahabari.

Kulingana na sheria hiyo, wale wanaoshiriki ushoga wanakabiliwa na adhabu kali ambayo inaweza kujumuisha kifungo cha maisha.
Mnamo Mei 29, 2023 Among alitangaza kuwa bunge litasimama kidete kukuza maadili ya watu wa Uganda.

Kwa upande mwingine, Benki ya Dunia mnamo Agosti, ilitangaza kuwa ingesitisha mikopo mipya kwa Uganda kufuatia hatua yake ya kuharamisha mapenzi ya jinsia moja.

Benki hiyo ilisema sheria hiyo inayoharamisha LGBTQ inakwenda kinyume na misingi na maadili yake ambayo hayabagui yeyote kwa misingi ya jinsia au rangi yake katika azma yake ya kukabiliana na umasikini duniani.

  • Tags

You can share this post!

Msimamizi wa Bajeti kushtakiwa kwa makosa anayodaiwa...

Mkenya aanza kutembea kilomita 500 kuchangisha pesa za...

T L