• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 3:17 PM
Wasioonyesha uzalendo kuadhibiwa nchini Zimbabwe

Wasioonyesha uzalendo kuadhibiwa nchini Zimbabwe

NA KITSEPILE NYATHI

HARARE, ZIMBAMBWE

BUNGE la Zimbabwe mnamo Jumatano lilipitisha sheria yenye utata ambayo inalenga kuwaadhibu raia “wasioonyesha uzalendo”.

Aidha, hatua hiyo ya kisheria inakinzana na ahadi ya Rais Emmerson Mnangagwa aliyotoa ya watu kuwa huru zaidi.

Chama tawala cha Rais Mnangagwa, ZANU-PF, kilitumia wingi wa wabunge wake kupitisha Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Jinai (Codification and Reform) 2022.

Mswada huo umejulikana sana kama Mswada wa Uzalendo.

Sheria ambayo imekuwa ikitumika tangu uchaguzi wa 2018 ilipitishwa siku iyo hiyo ambapo rais huyo mwenye umri wa miaka 80 alitangaza Agosti 23 kuwa tarehe ya uchaguzi mkuu. Uchaguzi huo unasubiriwa kwa hamu kubwa nchini humo.

Taarifa ya Baraza la Mawaziri mwaka 2022 ilisema: “Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Makosa ya Jinai (Mswada wa Marekebisho ya Kanuni na Marekebisho, 2022, unaongeza vifungu vya Sheria ya Makosa ya Jinai katika masuala yanayohusiana na mamlaka ya nchi hiyo kupitia kuharamisha mienendo ambayo inadhoofisha mamlaka ya Zimbabwe, utu, uhuru na maslahi ya taifa.”

Mswada huo sasa utawasilishwa kwa Seneti, ambayo pia inaongozwa na ZANU-PF, kabla ya Rais Mnangagwa kutia saini kuwa sheria.

Kando na hayo, Waziri wa zamani wa Fedha, Tendai Biti alisema Mswada huo unachukiza na kuulinganisha na sheria zilizopitishwa na utawala wa kikoloni wa Zimbabwe.

“Leo ni siku ya kusikitisha sana baada ya Bunge kupitisha Mswada wa Uzalendo jioni ya leo,” Bw Biti alisema mnamo Jumatano.

Aliongeza kwamba sheria hiyo mpya ni sheria ambayo haijawahi kushuhudiwa na ambayo inalenga kuzuia uhuru wa kujumuika, kukusanyika na kuzungumza kwa raia yeyote anayefanya mkutano na serikali ya kigeni.

Aidha Biti alihoji kwamba hata utawala wa ubaguzi kwa misingi ya rangi Rhodesia (jina la kikoloni la Zimbabwe) haukupitisha sheria hiyo ya kuchukiza.

Kadhalika, serikali imetetea sheria iliyopendekezwa kwa kulinganisha na Sheria ya Logan ya Marekani.

Sheria hiyo inaharamisha mazungumzo ya raia wasioidhinishwa na serikali za kigeni kuwa na mzozo na Amerika.

Ni watu wawili tu wamewahi kufunguliwa mashtaka ya kukiuka Sheria ya Logan na hakuna hata mmoja wao aliyehukumiwa.

Mchungaji Evan Mawarire, ambaye aliongoza maandamano yaliyotikisa utawala wa marehemu Robert Mugabe na kufungwa jela kwa uanaharakati wake, alisema sheria iliyopendekezwa ilikuwa shambulio dhidi ya uhuru wa kujieleza na kujumuika.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua: Wakenya wengi wanaamini mikakati ya Rais...

Rais apuuza itifaki za kijeshi na kuamuru waliofungiwa nje...

T L