• Nairobi
  • Last Updated October 1st, 2023 9:40 PM
Watu 288 wafariki baada ya treni tatu kugongana nchini India

Watu 288 wafariki baada ya treni tatu kugongana nchini India

NA AFP

TAKRIBAN watu 288 walifariki na mamia kujeruhiwa Ijumaa baada ya kutokea kwa ajali ya treni tatu zilizogongana nchini India, maafisa wamesema Jumamosi, hii ikiwa ajali mbaya zaidi ya treni kutokea nchini humo kwa kipindi cha miaka 20.

Mabaki ya treni hizo yametapakaa karibu na eneo la ajali mjini Balasore katika jimbo la mashariki la Odisha.

Matone ya damu yametapakaa kila mahali kwenye mabaki ya treni.

Mtafiti Anubhav Das ameambia AFP kwamba alikuwa ndani ya treni kwenye behewa la nyuma kabisa aliposikia sauti kali masikioni japo kwa umbali.

Behewa lake limesalia wima na akaruka nje bila jeraha.

“Nimeona matone ya damu, miili ikiwa imefinyika na pia mwanamume mmoja akiwa na jeraha baya mkononi akisaidiwa na mwanawe wa kiume,” amesema manusura huyo mwenye umri wa miaka 27.

“Nimesahau idadi kamili ya miili niliyohesabu kabla ya kuondoka kwenye eneo la ajali. Ninahisi kana kwamba nina hatia.”

 

Naye manusura mwingine Arjun Das amekiambia kituo cha televisheni cha Bengali kwamba alisikia sauti ya kishindo kabla ya kuanza kuona watu wakianguka. Ameruka hadi nje ya treni.

“Watu walikuwa wanapiga usiyahi, wakiomba usaidizi,” amesema.

Ajali ilitokea wakati treni kutoka mji wa kiteknolojia wa Bengaluru ikielekea Kolkata ilipotoka kwenye njia yake ya reli, na kuanguka kwenye reli nyingine. Dakika chache baadaye garimoshi la Coromandal Express likitoka Kolkata na kuelekea Chennai limegonga lile garimoshi la kwanza, huku mabehewa yake yakiyumba na kugonga treni la tatu lililokuwa limeegeshwa karibu na mahala hapo.

Shughuli za uokozi zinaendelea leo Jumamosi.

Mkurugenzi mkuu wa zimamoto Odisha Sudhanshu Sarangi amesema idadi ya walioangamia ni 288 ingawa inahofiwa huenda idadi ikapanda zaidi na hata kugonga 380.

“Watu wengi waliopelekwa hospitalini wanafariki na hata hapa tunaendelea kutoa miili zaidi kwenye mabaki,” Sarangi ameambia AFP.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ametua katika eneo la ajali kwa helikopta mnamo Jumamosi na alikuwa ameratibiwa kuwatembelea manusura waliolazwa katika hospitali kadha huko Balasore. Awali, Modi alikuwa ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba anahuzunika.

“Katika kipindi hiki kigumu, ninaomboleza na familia zilizopoteza wapendwa wao,” amesema Modi.

Akaongeza: “Waliojeruhiwa wapate afueni ya haraka.”

  • Tags

You can share this post!

Azimio wala njama kuyumbisha Mswada wa Fedha na usomaji wa...

Serikali yaonya walimu wanaosisitiza sare zinunuliwe...

T L