• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Zuma atakiwa ajiamulie kifungo anachotaka apewe

Zuma atakiwa ajiamulie kifungo anachotaka apewe

NA AP

ALIYEKUWA rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, ametakiwa kupendekeza kifungo ambacho angependa kupewa kwa kukwepa vikao vya mahakama.

Kiongozi huyo alikuwa amepewa hadi jana kutoa pendekezo hilo, kwa kukwepa msururu wa vikao vya mahakama kuhusu kesi yake kwa mashtaka ya ufisadi.

Zuma, 79, amekuwa akichunguzwa kuhusu sakata za ufisadi kwa miaka tisa ambayo alihudumu kama rais.

Amekuwa akikwepa vikao hivyo kwa kisingizio kuwa mwenyekiti wa jopo linaloendesha kesi dhidi yake amekuwa akimwonea. Tangu kesi hiyo ilipoanza, kiongozi huyo alitoa ushahidi mara moja tu mnamo 2019. Tangu wakati huo, amekuwa akisusia vikao vya jopo hilo.

Mnamo Januari 28, Mahakama ya Kikatiba nchini humo ilimwagiza Zuma kufika mbele ya jopo hilo, linaloongozwa na Naibu Jaji Mkuu Raymond Zondo. Hata hivyo, alipuuza agizo hilo.

Kutokana na hatua hiyo, Zondo aliiomba Mahakama ya Juu nchini humo kumfunga gerezani Zuma kwa miaka miwili kwa kukwepa vikao vyake.

Akionekana kutotishika, Zuma alikwepa tena kikao cha kwanza mwezi uliopita, huku akikosa kuwasilisha baadhi ya taarifa alizotakiwa.

Kutokana na hilo, mahakama sasa inamtaka Zuma kuamua “hatua anayopaswa kuchukuliwa” ikiwa atapatikana na hatia. Ijumaa iliyopita, Jaji Mkuu Mogoeng Mogoeng alimwagiza Zuma kuwasilisha taarifa isiyozidi kurasa 15 kufikia jana akielezea “aina ya kifungo ambacho angependa kupewa.”

Haijabainika ikiwa atazingatia agizo hilo. Kufikia jana, hakukuwa na taarifa yoyote kutoka kwake wala mawakili wake kuhusu agizo hilo. Wataalamu wanasema kuwa agizo hilo ni nadra sana kutoka kwa mahakama.

Kulingana na James Grant, ambaye ni wakili wa masuala ya kikatiba, agizo hilo linaonyesha kuna uwezekano mahakama inamchukulia Zuma kwa “hadhi” ikizingatiwa alihudumu kama rais.

Hata hivyo, aliongeza kuwa hilo halimaanishi hatapewa adhabu kali ikiiwa atapatikana na hatia. “Majaji wanajifanya wanyenyekevu ili kujaribu kumrai kushiriki moja kwa moja kwenye kesi hiyo. Huenda wanajitayarisha kumpa hukumu kali. Wanataka kuonyesha walimpa kila nafasi kujieleza,”akasema Grant. Omphemetse Sibanda, ambaye ni profesa wa sheria, alionya pendekezo hilo linaashiria mwelekeo mbaya kwa idara ya mahakama nchini humo.

“Mwisho wa mwelekeo huo ni kuwa kuna hatari kubwa mahakama “kutekwa” na kundi la wanasiasa na watu wenye ushawishi nchini. Chini ya hali hiyo, mahakama itatoa maamuzi yake kulingana na matakwa ya watu hao,” akasema.

Mapema mwaka huu, Zuma alifananisha mahakama nchini humo na utawala wa ubaguzi wa rangi ambao uliendeshwa na Wazungu katika miaka ya tisini.

Uasi wa Zuma umekigawanya chama tawala cha ANC katika kambi mbili, huku upande mmoja unaoongozwa na Rais Cyril Ramaphosa ukiapa kuendeleza harakati za kukabiliana na ufisadi.

You can share this post!

Wanaraga wa Kenya wanaocheza ughaibuni wafika 10

Faida za ‘beetroot’