Habari

Hacheki na Uhuru

June 9th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

JAJI Mkuu David Maraga, amejitokeza kuwa kiongozi pekee aliye na ujasiri wa kumwambia Rais Uhuru Kenyatta ukweli kuhusu vitendo vyake vinavyohujumu demokrasia na Utawala wa Kisheria.

Hii ni baada ya Rais Kenyatta kufanikiwa kuzima upinzani uliokuwa ukiongozwa na Raila Odinga, kufunga midomo ya wabunge na maseneta, kufifisha sauti za mashirika ya umma huku viongozi wa kidini wakienda mafichoni.

Lakini katika siku chache zilizopita, Jaji Maraga ametoa matumaini kuwa kuna mmoja aliyebaki kumtetea mwananchi wa kawaida.

Jumatatu, Bw Maraga alijitokeza akiwa na ukakamavu ambao haujaonekana nchini siku za majuzi, na kumwambia Rais Kenyatta kuwa vitendo vyake mbali na kuhujumu demokrasia, vinaweka msingi wa fujo kwa ukiukaji sheria hapa nchini.

Hii ni siku chache tu baada ya Jaji Mkuu kupuzilia mbali Agizo la Rais lililoonekana kutaka Idara ya Mahakama kuwa chini ya udhibiti wa Serikali Kuu.

Bw Maraga alimwambia Rais Kenyatta kuwa Idara ya Mahakama imebuniwa kikatiba na kamwe asiwe na mawazo kuwa anaweza kuipa maagizo kwani mamlaka yake hayatoki kwa Serikali Kuu mbali Katiba.

Kwenye taarifa kali Jumatatu, Jaji Maraga alimkashifu Rais kwa kupuuza maagizo mawili ya mahakama yaliyomtaka awaapishe majaji 41 walioteuliwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) mnamo Juni 2019.

“Ni lazima Mheshimiwa Rais nikukumbushe kuwa uliapa kulinda Katiba na sheria za Kenya. Nakuomba sasa uonyeshe kwa vitendo kuwa unaheshimu sheria kwa kutii maagizo ya mahakama,” akasema Jaji Maraga.

Alieleza kuwa tabia ya Rais Kenyatta kupuuza maagizo ya mahakama imekuwa mtindo katika Serikali Kuu.

“Kwa mfano, majuzi Serikali ilifukuza familia zaidi ya 1,000 katika mtaa wa Kariobangi jijini Nairobi bila kujali hatari ya Covid-19. Hii ni licha ya kuwepo kwa Agizo la Korti la kusimamisha ubomoaji wa makao ya wakazi hao.

“Serikali pia imekataa makusudi kulipa ridhaa ya zaidi ya Sh1 bilioni kwa waathiriwa wa ajali za barabarani zilizosababishwa na magari ya Serikali. Hii imewaacha waathiriwa hao katika shida nyingi.”

Alisema juhudi zake za muda mrefu za kushauriana na Rais Kenyatta kuhusu suala la uteuzi wa majaji 41 na upuuzaji wa Maagizo ya Korti zimegonga mwamba.

“Kwa muda mrefu nimejaribu kukutana nawe bila mafanikio ili tujadili masuala haya,” akasema Maraga.

Aliongeza kwa itakuwa ni kupuuza majukumu yake “iwapo sitazungumza kuhusu machungu anayopitia ‘Wanjiku’.”

Jaji Mkuu alisema Serikali inaweka msingi wa upotovu nchini inapopuuza sheria, kwani inaweka mfano mbaya kwa wananchi kuiga mtindo huo.

“Serikali inapaswa kuwa mstari wa mbele kuheshimu sheria. Haiwezi kutarajiwa wananchi watii sheria iwapo yenyewe inakiuka sheria hizo bila kujali.

“Serikali yenyewe inahujumu Utawala wa Kisheria kwa kupuuza Maagizo ya Korti. Mtindo huu ni hatari kwa demokrasia yetu kwa sababu inaweza kuchochea mlipuko wa uvujaji wa sheria,” akaeleza.

Kulingana na Bw Maraga, wananchi wanaotafuta haki mahakamani hawawezi kuhudumiwa kwa wakati ufaao na haraka kutokana na uhaba wa majaji, kiini kikiwa ni Rais Kenyatta kupuuza Maagizo ya Korti ya kuapisha majaji hao 41.

Vitengo vya mahakama ambavyo vimeathirika zaidi ni Mazingira na Ardhi, Rufaa pamoja na Uajiri na Leba.

“Ni muhimu kuweka wazi kuwa uhaba huu wa majaji pamoja na kulemazwa kwa shughuli za mahakama kumesababishwa na Rais mwenyewe kwa kukataa kuapisha majaji 41 walioteuliwa na JSC. Rais ameendelea kukataa kuwaapisha majaji hao licha ya korti mbili tofauti kumwagiza afanye hivyo,” akasema Jaji Maraga.

Alipokataa kuwaapisha majaji hao, Rais Kenyatta alidai kulikuwa na baadhi yao wanaoshukiwa kuhusika katika uhalifu.

Lakini Jaji Maraga alimkosoa akisema hata baada ya kuitisha ushahidi wa madai hayo hajapokea majibu yoyote.

Alisema kuwa kulingana na Katiba, Rais hana mamlaka yoyote ya kukataa kuteua majaji hao, na hivyo hatua yake ni kukiuka Katiba aliyoapa kulinda na kutetea.

“Katiba haimpatii Rais mamlaka yoyote kuhusu orodha ya uteuzi kutoka kwa JSC isipokuwa kuwateua na kuwaapisha,” akasema Jaji Maraga.