Hadhi: Wito serikali iimarishe majukwaa ya kazi za sanaa Nakuru

Hadhi: Wito serikali iimarishe majukwaa ya kazi za sanaa Nakuru

Na RICHARD MAOSI

WASANII kutoka Nakuru Arts Players Theatre, wanatumai kuwa serikali ikiongozwa na rais itasaidia kuboresha miundomsingi ya kazi za sanaa, Nakuru inapokaribia kupata hadhi ya kuwa jiji.

Kwa kiasi fulani hatua hii itasaidia kutoa nafasi sawa kwa wasanii wa Nakuru kama ile wanaopata wale wanaotokea Kisumu, Mombasa na Nairobi.

Aidha ni hatua ambayo italeta mshikamano baina ya wasanii, na kuwapatia uwezo wa kumiliki vyombo vya sanaa, mbali na kutengeneza kumbi kadhaa za burudani, kwa vijana wenye talanta.

Ni habari za kutia moyo ingawa wasanii wengi bado hawajaona jambo la kujivunia miaka 58 baadaye tangu Kenya ijinyakulie uhuru na kupata madaraka, baadhi wakidai kuwa hatua yenyewe imeharakishwa.

Tulitembelea nguli wa michezo ya kuigiza ya jukwaani kutoka Nakuru Players Theatre Bw Jackson Oloo ambaye anasikitika kuwa, bado taifa halijakumbatia ipasavyo mchango wa wao katika jamii.

Akizungumza na Taifa Leo, alisema vipaji vingi vimekuwa vikiozea mitaani, licha ya rais kuunda jopo la kushughulikia wasanii mnamo 2020.

Kulingana naye wasanii wadogo wana changamoto nyingi, ikiwemo ni pamoja na kunyimwa shoo, kutokuwa na mameneja wa kuwasimamia na mapromota wanaowapunja kwa jina la kuwatengenezea majina.

Alieleza kuwa watumbuizaji wengine wamekata tamaa, baada ya kuingiwa na kasumba kuwa ni lazima mtu aonekane kwenye runinga akitaka kupata umaarufu wa kutambulika.

“Hatuna mashirika ya kusimamia wasanii wala kuwapatia ushauri nasaha namna ya kuweka akiba ya kujisimamia, wengi wetu tumebaki kutengeneza majina na uzoefu ,” akasema.

Kwingineko Monica Muthoni mwigizaji wa makala ya fasihi kwa shule za upili anasema janga la covid-19 , lilikuja na hasara nyingi kuliko faida.

Anasema sanaa ya kuigiza inategemea ukumbi wa maonyesho na hadhira kubwa, lakini tangu kisa cha kwanza kutangazwa mnamo 2020, kundi lake liliahirisha maonyesho yote.

“Imekuwa ni wakati mgumu kwa wasanii ambao wanategemea uigizaji, hali ambayo iliwaongezea wasanii wengi mzigo wa kimaisha,” akasema.

Alieleza kuwa ni hali iliyokuja na mabadiliko ya kitabia na kanuni za kawaida, watu wengi wakianza kufanyia kazi majumbani pao, wasije wakatangamana kwenye kumbi za maonyesho.

“Tulikuwa tukitengeneza hela nzuri wakati wa kusherehekea sikukuu za Kitaifa kama vile siku ya Madaraka na Jahmhuri Dei,” alifafanua.

You can share this post!

Colombia wapepeta Ecuador 1-0 kwenye pambano la kuwania...

Familia yahangaika baada ya kupata mwili uliokuwa umetoweka...