Makala

HADITHI: Sindwele na Pengo wawapa wenzao ‘maagano spesheli’

February 25th, 2020 2 min read

NA SHIUNDU MUKENYA

SHUGHULI za kawaida zilianza kuchukua sura tena baada ya likizo fupi. Shuleni Sidindi, shughuli ziling’oa nanga Jumatatu asubuhi.

Hata hivyo, baadhi ya walimu hawakuwasili Jumatatu hiyo kwani nao walikuwa wamewapeleka watoto wao shuleni.

Hawa walitua Jumanne. Kinyume na matarajio, walimu wawili walikuwa hawajawasili kufikia Jumanne hiyo, hili halikutarajiwa kabisa. Ilisadifu kuwa wawili hawa walikuwa wale mabinti waliokuwa na miadi na Pengo kule Camp David.

Walimu wetu walipofika shuleni hatimaye, nyuso zao zilidhihirisha kusawijika. Walipoulizwa kilichowasawijisha, walisingizia mavune ya likizo fupi.

Ilipofika zamu ya Pengo kuwaamkua walimu hao, waliupuuza mkono walionyooshewa. Akalazimika kuwaamkua kwa kauli tu.

Walimu wetu walimpa Pengo salamu za shingo upande kwa sauti ya chini mno na ya kujilazimisha. Ilikuwa tu bahati kuwa walimu wengine walikuwepo, vinginevyo Pengo aliamini kuwa hawangezijibu salamu zake.

Akashuku kuwa kusawijika huko kulitokana na miadi yao iliyokwenda tenge wakati wa likizo fupi.

Pengo aliamini kuwa yaliyotukia wakati wa likizo fupi yalitokana na usodai na uchakaramu wa Sindwele.

Ni yuyo huyo Sindwele aliyekuwa nyakanga wa mizungu ya wana wa dunia hii kama Sindwele na wenzake walivyojitapa. ‘Waama hawa si wana wa dunia tu! Hawa ni wana wa giza haswaa!’ Pengo alijiambia.

Papo hapo, darubini yake ikarejea nyuma kumkumbusha yaliyotukia siku hiyo baada ya miadi yao kule Camp David.

Mabinti hao walikuwa wamegusagusa chakula walichoagiza na kilichogharamiwa na Pengo. Sindwele akaahidi kugharamia nauli. Alipiga simu kumwita dereva wa teksi.

Likaja gari moja kachara lililowachukua mabinti hao. Dereva wa gari hilo alinong’onezana na Sindwele faraghani kisha akaondoka na mabinti hao.

Punde tu walipoondoka, Sindwele alimwambia Pengo kuifunga simu yake hadi kesho yake.

Pengo ambaye hadi wakati huu alikuwa kamkabidhi Sindwele hatamu za kuendesha miadi ya siku hiyo aliufyata tu na kufwata aliloambiwa na Sindwele.

Alipoifungua simu kesho yake alikutana na jumbe tumbi nzima kwenye kikasha cha ujumbe. Nyingi ya jumbe hizi yalikuwa matusi yaliyoelekezewa Pengo na Sindwele. ‘Pamoja na uchochole wenu, mumefunguka skrubu za akili.’

Aliandika mmoja wa mabinti hao. Alipoyapeleleza, ndipo alipoambiwa kuwa kumbe Sindwele hakuwa kalipia nauli ya wasichana hao kama alivyoahidi, dereva wa gari hilo kachara aliwajia juu wasichana hao na kuwalazimisha kulipia nauli yao.

Pengo alipojaribu kushauriana na Sindwele kuihusu hili, Sindwele alimwambia kuwa mabinti hao walistahili kuuhisi uzito wa gharama.