Makala

HADITHI YA WIKI: Uchambuzi wa ‘Mlinzi na chekechea yake’

November 4th, 2020 2 min read

Waandishi: Ursula Wafula na Nina Orange

Mchapishaji: African Storybooks Initiative

Mhakiki: Wanderi Kamau

Kitabu: Novela ya Watoto

Mtafsiri: Ursula Wafula

Jina la Utungo: Mlinzi na Chekechea Yake

HAMJAMBO watoto? Je, huwa mnawatunza wanyama au mnawatesa? Je, mnafahamu kwamba wanyama ni sehemu ya uumba wake Mungu ambao tunapaswa kuulinda?

Utunzaji wa wanyama ni mojawapo ya mambo ambayo huonyesha hali ya kujali miongoni mwa wanadamu.

Hadithi ‘Mlinzi na chekechea yake’ inaonyesha mfano bora tunaopaswa kuiga katika kuwalinda wanyamapori, hasa nyakati hizi ambapo wanakabiliwa na tishio la kuangamia kabisa duniani.

Hadithi hii inaonyesha mwendelezo wa wito ambao umekuwa ukitolewa na serikali na taasisi zingine zinazowatetea wanyama kuhusu umuhimu wa kuwasaidia.

Inamhusu mlinzi aliyeendesha chekechea yake maalumu kwa ushirikiano na wafanyakazi wake kuwasaidia wanyama mayatima, ambapo baadaye waliwaruhusu kurejea msituni baada ya hali zao kuimarika.

Mnyama wa kwanza aliyefika katika chekechea hiyo maalumu ni Mkite. Alikuwa mtoto wa tembo, mwenye umri wa mwaka mmoja.

Mlinzi na wasaidizi wake walimhurumia kwa sababu alikuwa amekonda na mwenye huzuni sana.

Siku chache baadaye, afya yake iliimarika ambapo alianza kucheza na wanyama wengine aliowakuta kwenye chekechea hiyo.

Baada ya siku kadhaa, helikopta ilitua katika chekechea hiyo ikiwa imembeba mtoto mwingine wa tembo. Alikuwa amedhoofika sana. Walimhurumia kwani alionekana akiwa mnyonge.

Yatima huyo aliitiwa Ndiwa. Alikuwa na umri wa miezi mitano tu. Walimnywesha maziwa ili kuimarisha hali yake kiafya.

Yatima wa tatu kufika kwenye kituo hicho aliitwa Malea, ambaye ni kifaru. Alikuwa na umri wa miezi sita.

Kituoni humo, Malea alikutana na yatima aliyeitwa Enkare, ambaye alikuwa nyati mdogo. Wawili hao wanaibukia kuwa marafiki wakubwa kwani walitembea kila mahali pamoja.

Wanyama wengine waliopelekwa katika chekechea hiyo na kupata usaidizi ni mtoto wa twiga aliyeitwa Ambia. Kama wale wengine waliotangulia, alikuwa mnyonge sana ingawa anasaidiwa pakubwa na wasaidizi wa Mlinzi wa Chekechea kwa kumpa chakula.

Kituo pia kiliwasaidia swara mapacha; Abei na Moit, waliofika humo wakiwa wanyonge sana kwani walikuwa wamezaliwa siku chache tu kabla. Hata hivyo, mkasa unatokea wakati Moit anapofariki.

Kituo kiliwapokea na kuwasaidia watoto wa simba waitwao; Kopi, Kepi na Keji. Cha kushangaza ni kwamba, walinzi waliwatunza wanyama hao bila mapendeleo yoyote. Hali za mayatima hao zilipoimarika, waliwarejesha porini kuendelea na maisha yao kama kawaida.

Bila shaka, hadithi hii inatuonyesha kuwa mwanadamu pia anaweza kuchangia katika kuimarisha hali na mazingira wanayoishi wanyama. Si lazima uhusiano wake na wanyama uwe mbaya hata kidogo.

Ni hadithi yenye michoro ya kuvutia, hali inayomvutia na kuifanya iwe rahisi kusomeka na kila mmoja.

Ni hadithi ambayo pia inatufunza kuhusu umuhimu wa kuwajali na kuwasaidia wale walio karibu nasi, kama anavyofanya Mlinzi na wasaidizi wake kwa wanyama mayatima.

Soma hadithi hii au itazame katika runinga yako ya NTV kila Jumatatu kuanzia saa moja na dakika 50 usiku.

[email protected]