Hafla ya kufuzu kwa mahafali 5,000 yafana chuoni MKU

Hafla ya kufuzu kwa mahafali 5,000 yafana chuoni MKU

NA LAWRENCE ONGARO

WAHITIMU wapatao 5,000 wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya wamehimizwa kushika usukani mara moja na kubuni kazi zao wenyewe bila kutegemea serikali.

Katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kati, Dkt Peter Mathuki, alisema  kujumuishwa kwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuwa sehemu ya jumuiya ni hatua ya kusifiwa kwa sababu uchumi wa nchi wanachama wa Afrika Mashariki na kati utaimarika pakubwa.

“Yeyote aliye na ujuzi wake ana nafasi kubwa ya kuzuru nchi yoyote ile katika muungano na kutafuta jinsi ya kubuni biashara. Jambo hilo ni muhimu sana hasa kwa wahitimu waliokamilisha masomo yao leo (jana Ijumaa),” alifafanua Dkt Mathuki.

Alisema hali ya biashara itaimarika pakubwa na pia hivi karibuni kutakuwepo na sarafu moja itakayotumika katika nchi zote wanachama.

Alipongeza MKU kwa kuwa miongoni mwa vyuo vikuu ambavyo vimepiga hatua kwa kufungua vitengo kadha katika nchi jirani kama Uganda, na Rwanda.

Hafla ya kufuzu kwa mahafali 5,000 ilihudhuriwa na wakuu wa MKU miongoni mwa wageni wengine. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Mwanzilishi na mwenyekiti wa chuo hicho Profesa Simon Gicharu ame watahadharisha vijana wanaokimbilia uarabuni kuwa ni sharti wachunguze vizuri kabla ya kusafiri.

“Inasikitisha sana kuona ya kwamba vijana wengi wanafikiri kuwa kwenda ng’ambo ni Jambo la kufurahia. Lakini ningetoa tahadhari  Kwanza wafanye uchunguzi ili wajue  ni mahali ipi nanakokwenda,” alifafanua Prof Gicharu.

Alisema MKU imefanya makubaliano ya kufanikisha wanafunzi wanaosomea udaktari wasafiri Ujerumani ili pia kujionea mafunzo ya nchi hiyo.

Alisema kwanza watalazimika kuelewa lugha ya Kijerumani ili kuweza kuendelea na masomo yao.

Alisema wanafunzi hao wanastahili kuzuru chuo cha Hochschle Koblenz ambapo wataweza pia kupata ajira kama madaktari na wauguzi.

Aliwahimiza pia wahitimu waliokamilisha masomo yao wajisajili kupata mikopo kutoka kwa hazina ya Hustler Fund ili kuanzisha biashara ndogo kabla ya kuendelea kwa kubwa.

“Ni vizuri kuanza na kidogo kabla ya kupanda na kutafuta biashara kubwa,” alisema Prof Gicharu.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Chansela wa chuo hicho Prof John Struthers akiandamana na Naibu Chansela Prof Deogratius Jaganyi.

Wengine waliohudhuria ni wageni mashuhuri na wahadhiri wa chuo hicho.

Wazazi wakihudhuria hafla hiyo iliyofana sana huku wakishukuru chuo hicho kwa kuwapa mafunzo kamili wana wao.
  • Tags

You can share this post!

Mpango maalumu wa Rais kupanda miti kwa ajili ya uhifadhi...

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Argentina sasa kuvaana na Croatia...

T L