Habari za Kaunti

Hafla za mazishi Kisii zageuzwa jukwaa la viongozi kurushiana matusi

February 11th, 2024 2 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

WANASIASA na viongozi wa mirengo kinzani kutoka Kaunti ya Kisii sasa wameanza kugeuza hafla za mazishi majukwaa ya kupigiana kelele kutumia wahuni.

Hafla hizo ambazo kimsingi zinafaa kuwa za kufariji familia zilizofiwa na wapendwa wao, sasa zinatekwa na wanasiasa wanaojibidiisha kuonyesha ubabe wao joto la siasa likizidi kuongezeka eneo hilo.

Mnamo Februari 9, 2024, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alilazimika kukatiza hotuba ya rais, aliyokuwa akiisoma katika mazishi ya Mwalimu Mkuu wa Chuo cha Kiufundi cha Kisii Daniel Nyariki, baada ya kupigiwa kelele na wahuni wakati gavana wa Kisii Simba Arati alikuwa akiingia mazishi hayo.

Akionekana kukerwa na hatua hiyo iliyomfanya asitishe kusoma hotuba ya rais mara kwa mara, Bw Machogu alimnyoshea Arati kidole cha lawama akimshutumu kwa kuchochea kuzomewa kwa viongozi wengine katika hafla kama hizo.

Mbunge huyo wa zamani wa Nyaribari Masaba alidokeza kuwa uhuni kama huo ulikuwa kinyume na utamaduni wa jamii za Kiafrika ambapo hafla za mazishi zinafaa kuwa za kutoa heshima kwa waliofiwa na hata marehemu .

“Tuhahudhuria mazishi ili kuomboleza walioaga na kuwafariji waliofiwa na sio kusafirisha vijana waje kupigana na kuwazomea viongozi wengine wakati wa kuzungumza mazikoni,” waziri Machogu alisema na kisha akaondoka na kumwacha Bw Arati katika mazishi hayo.

Gavana Arati aliposimama kuhutubu, alimdhihaki Bw Machogu na kusema hana umaarufu wowote katika gatuzi hilo.

Mbunge huyo wa zamani wa Dagoretti Kaskazini alikana kwamba ni yeye aliyewalipa raia hao waliozomea baadhi ya viongozi waliofika chuoni humo kumpa Nyariki buriani ya mwisho.

Alitolea mfano jinsi alipomshinda Machogu kinyang’anyiro cha ugavana wa Kisii kwenye uchaguzi wa 2022 na akamwalika ashindane naye tena mwaka 2027.

“Anafaa kumshukuru rais kwa kumwonea huruma alipomteua serikalini. Alimtoa kwenye magofu baada ya mimi kumpa kishindo kikubwa. Hafai kusimama hapa kunishtumu,” gavana Arati alijipiga kifua.

Mbunge huyo wa zamani wa Dagoretti Kaskazini alikana kwamba ni yeye aliyewalipa raia hao waliozomea baadhi ya viongozi waliofika chuoni humo kumpa Nyariki buriani ya mwisho.

Kwa muda mrefu, Bw Arati amekuwa akimlaumu Bw Machogu kwa kudai anashirikiana na Mbunge wa Mugirango Kusini Sylvanus Osoro kumhangaisha.