Kimataifa

Haiti: Biden amrai Ruto kutuma polisi haraka

May 27th, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

RAIS wa Amerika, Joe Biden amehimiza Kenya kufanya hima kutuma vikosi vyake vya usalama nchini Haiti baada ya kutokea mauaji ya wamishenari watatu wanaofanya kazi na kundi la Amerika katika taifa hilo linalokumbwa na michafuko.

Wito huo ulijiri Ijumaa punde baada ya Shirika la Kimisheni Haiti kutangaza kuwa wamishenari wake watatu walipigwa risasi na kuuawa na washambuliaji waliobeba bunduki Alhamisi usiku katika jiji kuu la Port-au-Prince.

Mauaji hayo ndiyo ya hivi karibuni katika miezi kadhaa ya ghasia zinazozidi kuongezeka Port-au-Prince, ambayo bado inadhibitiwa na makundi ya waasi sugu ambao wametekeleza misururu ya mashambulizi makali kote jijini humo.

Haya yalijiri vilevile Rais wa Kenya William Ruto alipokuwa akikamilisha ziara yake katika jiji la Washington, DC, ambapo alikutana na Biden na viongozi wengine wakuu Amerika kujadili masuala anuwai ikiwemo operesheni ambayo imesitishwa kwa muda mrefu ya kutuma vikosi Haiti.

“Hali ya usalama Haiti haiwezi kusubiri,” Msemaji wa Baraza la Kitaifa kuhusu Usalama alisema Ijumaa.

Alisema Biden aliahidi kuunga mkono “mchakato wa kutuma upesi” vikosi vinavyoongozwa na Kenya aliposhiriki mazungumzo na Ruto Alhamisi. Tunatuma rambirambi zetu kwa familia za waliouawa wakati huu wa majonzi,” alisema Msemaji akirejelea wamishonari.

Mbunge wa Jimbo la Missouri, Ben Baker, alifichua Ijumaa kuwa binti yake, Natalie Lloyd, na mkaza mwanawe, Davy Lloyd, ni miongoni mwa waliouawa.

Wawili hao wamekuwa wakifanya kazi kama wamishonari nchini humo ambapo Davy Lloyd ni mwanawe waasisi wa Kampuni ya Misheni Haiti, David na Alicia Lloyd, walioanzisha shirika hilo 2000.

Mtu wa tatu aliyeuawa hajatambulishwa.

Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada ya kibinadamu yamekuwa yakihimiza msaada zaidi kutolewa kwa raia wa Haiti.

Kenya imeahidi kutoa maafisa 1,000 kushiriki operesheni hiyo ya UN inayofadhiliwa pakubwa na Amerika na inayolenga kuzima magenge ya waasi.

Operesheni hiyo inatazamiwa hatimaye kujumuisha maafisa 2,500.

Haijabainika operesheni hiyo itaanza lini baada ya maafisa kusema ingezinduliwa wakati sawa na ziara ya Rais Ruto Amerika.

Duru ambazo hazikutajwa ziliripotiwa zikisema Alhamisi kwamba operesheni hiyo imecheleweshwa.

Aliyekuwa balozi wa Amerika, Haiti, Daniel Foote, ambaye amegeuka mkosoaji wa sera za utawala wa Biden, alieleza vyombo vya habari wiki iliyopita kwamba azma ya operesheni hiyo imezingirwa na utata.

Raia wengi wa Haiti vilevile wanatilia shaka vikosi vya kigeni kuingilia kati baada ya oparesheni zilizofanyika mbeleni kushindwa kurejesha utulivu au kuangazia matatizo yanayokumba taifa hilo.

Hivi majuzi, kikosi cha UN cha kudumisha amani Haiti kilihusishwa na mlipuko mbaya wa kipindupindu na madai ya dhuluma za ngono.

Akijibu swali kuhusu operesheni ya kutuma vikosi Haiti, Ruto alisema Alhamisi kuwa Kenya “inaamini wajibu wa amani na usalama popote duniani, ikiwemo Haiti, ni jukumu la mataifa yote”.