Habari Mseto

Haji aagiza maafisa 7 wa Homa Bay kukamatwa

August 16th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

MKUU wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji Alhamisi alielekeza Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuwatia nguvuni maafisa saba wa kaunti ya Homa Bay, kufuatia kutoweka kwa Sh26 milioni.

Katika barua iliyochapishwa kwenye akautni ya Twitter ya Bw Haji, karani wa bunge la kaunti hiyo Otieno Bob Kephas pamoja na baadhi ya wawakilishi wa wadi na maafisa kwenye idara za fedha na ununuzi wanatuhumiwa kufuja pesa hizo kwa kununua huduma hewa.

Maelekezo hayo yalikuja baada ya tume ya EACC kuwachunguza maafisa husika na kupendekeza kushtakiwa kwao, ikisema walitumia mamilioni ya pesa za kaunti kununua huduma dhahania kwenye vipindi vya miaka ya fedha 2014/15 na 2016/17.

“Uchunguzi wa EACC ulibaini kaunti ya Homabay ilipuja pesa kupitia kununua huduma za hoteli na kuwalipa wawakilishi wodi marupurupu ambayo hayakufaa, hivyo kukitokea hasara ya Sh26,872,278,” ikasema barua hiyo, iliyotiwa sahihi na DPP.

Kupitia barua ya Juni 12, 2018 EACC ilikabidhi DPP barua iliyopendekeza kukamatwa kwa washukiwa hao saba na kushtakiwa kwao kwa jinai za kiuchumi.

“Nimeikagua faili hiyo na nimeridhika kuwa watu waliotajwa humo walihusika moja kwa moja kutekeleza makossa yanayodaiwa na hivyo wanapaswa kushtakiwa,” akasema Bw Haji.

Kwenye barua hiyo, DPP aliendelea kuamuru EACC kuwakamata Bw Otieno Bob Kephas, Michael Owino Ooro, Isaac Ouso Nyandege, Judith Akinyi Omongi, Caroline Sang, Morris Odiwuor Amek na Edwin Omondi Okollo mara moja, akiongeza kuwa afisi yake inaandaa mashtaka dhidi yao.