Habari Mseto

Haji aagiza Obado akamatwe

August 26th, 2020 1 min read

Na JUMA NAMLOLA

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji ameagiza Gavana wa Migori, Okoth Obado akamatwe kuhusiana na ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za kaunti.

Kwenye taarifa Jumanne, Bw haji alisema uchunguzi uliofanywa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ulithibitisha kwamba Bw Obado alipokea Sh73,474,360 milioni kupitia kwa watu waliomwakilisha na pia wafanyakazi wa serikali ya kaunti.

“Baada ya uchunguzi, ilibainika kuwa Bw Obado alitumiwa zaidi ya Sh73 milioni na watu mbalimali. Aidha, kampuni zilizopewa tenda hatimaye uchunguzi ulionyesha wakurugenzi ni watu wa karibu wa gavana huyo,” akasema.

Pia, ilifichuka kuwa kampuni 12 zilituma karibu Sh39 milioni kwa akaunti za watoto wa Bw Obado ambao walitajwa kuwa Achola Dan Okoth, Susan Scarlet Okoth na Jerry Zachary Okoth.