Habari Mseto

Haji kubatilisha uamuzi wa kuwaachilia wanajeshi 25 waliopangiwa kunyongwa

October 13th, 2018 2 min read

 PHILIP MUYANGA na CHARLES WASONGA

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji ameruhusiwa kuwasilisha rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuwaachilia huru wanajeshi 25 waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa na mahakama ya kijeshi.

Mahakama ya Rufaa ilisema kuwa DPP ana haki ya kupinga aumuzi wa Mahakama Kuu wa kuwaachilia huru wanajeshi hao ambao walikuwa wameshtakiwa kwa kushindwa kutelekeza majukumu yao.

Jopo la majaji  Alnashir Visram, Wanjiru Karanja na Martha Koome wa mahakama ya rufaa walisema kuwa haki hiyo haitokani Sheria wa Jeshi la Kenya (KDF) iliyofanyiwa mabadiliko kwa sababu utekelezaji wa sheria hiyo haiwezi kufanywa kuanzia nyuma kwa sababu haki hiyo inatambuliwa na katiba.

“Kwa sababu sheria ya KDF sasa imefanyiwa mabadiliko, hakuna sheria ambayo inamnyima mwasilishaji ombi (DPP) haki ya kuwasilisha rufaa katika mahakama hii kuhusiana na rufaa ya pili kuhusu masuala yaliyotoka katika Mahakama ya kijeshi,” wakasema majaji hao.

Watatu hao walisema wanaamini kuwa sheria ya KDF ilitafanyiwa mabadiliko ili kuifanya iwiane na Katiba kwa ajili ya kumpa DPP haki, sawa na watu wengine, ya kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Rufaa dhidi ya rufaa ya pili kuhusu masuala yaliyoibuka kutoka mahakama ya kijeshi.

Majaji Alnshir Visram, Wanjiru Karanja na Martha Koome walimpa Bw Haji muda wa siku 14 kuwasilisha rufaa yake.

DPP alikuwa amewasilisha ombi akisema kuwa Sheria ya KDF ya 2012 (iliyofanyiwa marekebisho) haikuelezea utaratibu ambao unafaa kutumiwa na upande wa mashtaka unapotaka kuwasilisha rufaa.

Kulingana na  Bw Haji rufaa anayotarajia kuwasilisha inalenga kuibua masuala ambayo yanapasa kushughulikiwa na mahakama hiyo.

Upande wa mashtaka ulikuwa umedai kuwa uamuzi wa kuwaachilia huru wanajeshi hao ulikuwa na athari ya kuhujumu mamlaka ya mahakama ya kijeshi kama asasi ya kudumisha nidhamu jeshini, hali ambayo inaweza kuathiri usalama wa nchini.

Kupitia mawakili wao, wanajeshi hao walisema kuwa ombi la DPP linahujumu utendekazi wa mahakama na hauna maana yoyote.

Mnamo mwaka wa 2015, Jaji wa Mahakama Kuu Martin Muya aliwaachilia huru wanajeshi wa zamani wa kikosi cha wanamaji akisema kosa la kutekeleza majukumu yao haikuthibitishwa.