Haki Africa yazindua kituo cha kufuatilia uchaguzi

Haki Africa yazindua kituo cha kufuatilia uchaguzi

NA JURGEN NAMBEKA

SHIRIKA la kutetea haki za binadamu la Haki Africa, limezundua kituo cha kupeperusha habari wakati wa Uchaguzi Mkuu ili kuwawezesha Wapwani na Wakenya kwa ujumla kufuatilia yatakayojiri kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa wiki ijayo.

Akizungumza wakati wa mahojiano na waandishi wa habari katika makao makuu ya shirika hilo jijini Mombasa, Mkurugenzi Mkuu wa Haki Afrika Hussein Khalid alieleza kuwa kituo hicho cha habari kitapeperusha habari katika mitandao baada ya kuzikagua na kuhakikisha ni za kweli.

“Leo tumezindua kituo chetu cha kufuatilia matukio mbalimbali ya uchaguzi wa wiki ijayo. Hatusemi kuwa kutazuka vurugu ila tunataka kuwapa wakazi wa Pwani na Kenya nzima kwa ujumla uwezo wa kupata habari endapo lolote litatokea,” alisema Bw Khalid.

Huku zikisalia siku mbili uchaguzi uandaliwe, kituo hicho kitapokea habari kutoka kwa maafisa zaidi ya 220 walioidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka kama waangalizi wa Uchaguzi.

Msimamizi wa masula ya mawasiliano katika Haki Africa Bw Hateeb Mohammed alieleza kuwa, kituo hicho ambacho kitafanya kazi kwa muda wa saa 24 kitawawezesha pia Wapwani wanaokabiliwa na changamoto zozote zinazotokana na uchaguzi, kupata huduma za dharura.

“Kuna nambari zetu za simu zisizolipishwa ambazo waweza kupiga kama Mkenya na utapata usaidizi wa dharura. Pia mitandao yetu ya kijamii itakuwa na habari zilizochunguzwa ili Wapwani wasiamini habari zozote zitakazowekwa wenye mitandao ya kijamii,” alieleza Bw Mohammed.

Bw Khalid aliwataka Wapwani kupiga kura kwa amani akionya dhidi ya kutumika vibaya na viongozi kwa manufaa yao.

  • Tags

You can share this post!

Chebukati awasihi Wakenya kuombea maafisa wa IEBC

DOUGLAS MUTUA: Usichague wenye ndimi telezi bali unaowaamini

T L