Habari Mseto

HAKI MITANDAONI: Dume lililotwanga mke mjamzito labambwa

August 14th, 2018 1 min read

NA PETER MBURU

MAMA mjamzito aliyedaiwa kujeruhiwa vibaya na mumewe, baada ya kuchapwa alipomcheleweshea chakula ameruhusiwa kutoka hospitalini.

Bi Valarie Masibo, 29 wa mtaa wa Kipkaren, Eldoret sasa anauguza majeraha ya usoni, kwenye masikio na meno, akidaiwa kuchapwa na Bw Naftali Luzeli wa miaka 26.

Hata hivyo, polisi walimkamata mshukiwa na anazuiliwa katika kituo cha Yamumbi, baada ya picha za mdhulumiwa kusambaa mitandaoni.

Inadaiwa kuwa sababu ya jamaa huyo kuchukua hatua hiyo ya kinyama ilitokana na mkewe kuchelewesha chakula cha jioni.

“Mshukiwa yumo mikononi mwetu na atafikishwa mahakamani kushtakiwa kwa kumdhulumu mtu punde tu ripotu ya daktari ikiwasilishwa,” mkuu wa polisi eneo la Eldoret Kusini Wilson Abduba.

Alisema mama huyo alipelekwa hospitali ya rufaa ya Moi iliyoko Eldoret kupokea matibabu.

Kulingana na shangaziye Bi Msibo, Rosemary Kusimba, wanandoa hao wamekuwa na matatizo ya kila mara, huku Bw Luzeli akidaiwa kumchapa mkewe kila wanapokorofishana.

“Bi Masibo hajawahi kufurahia ndoa tangu aolewe miezi mitano iliyopita. Juhudi zetu za kuwapatanisha hazijafaulu,” akasema Bi Kusimba.

Alisema mshukiwa alikuwa ametoa Sh500 za kununua chakula lakini alipofika nyumbani chakula hakikuwa tayari, ndipo akamwangukia mkewe kwa kichapo.

“Inadaiwa kuwa alikuwa mlevi, alitumia kuni kumchapa Bi Masibo na alimjeruhi vibaya kabla ya kuokolewa na majirani waliomkimbiza hospitalini,” Bi Kusimba akasema.

Mama huyo, hata hivyo aliruhusiwa kutoka hospitalini lakini anaishi kwa Bi Kusimba akizidi kupata nafuu.