Habari za Kitaifa

Haki ya kikatiba ya elimu yageuka ndoto

February 2nd, 2024 3 min read

NA DAVID MUCHUNGUH

MPANGO wa elimu bila malipo ulioanzishwa na Rais wa Tatu Kenya, Mzee Mwai Kibaki mnamo 2003 na kujumuishwa kwenye Katiba ya 2010 umeonekana kuchukua mkondo tofauti na kuwaacha wadau katika sekta ya elimu kwenye njia panda.

Udadisi uliofanywa na Taifa Leo unaashiria kuwa, Wakenya wamelazimika kubeba mzigo mzito wa kuwasomesha watoto wao katika shule za umma huku wanafunzi kutoka familia maskini wakinyimwa haki yao ya kikatiba kupata elimu.

Wasimamizi wa shule vilevile hawajanusurika kutokana na masaibu hayo.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanyiwa bajeti, mgao wa fedha, idadi ya watoto wanaojiunga na shule ikilinganishwa na bei halisi ya bidhaa na vyakula kwa sasa imepanda.

Wanafunzi katika shule za kutwa hulipia chakula kupitia maafikiano baina ya walimu na bodi za usimamizi.

Shule zimeathirika zaidi kwa sababu haziruhusiwi kutoza ada za ziada, hali ambayo imeathiri shughuli huku bodi za usimamizi zikihangaika kuajiri walimu ili kuziba pengo la uhaba wa walimu unaoathiri karibu shule zote.

Taifa Leo imebaini kuwa, mwongozo kuhusu karo inayolipwa na wazazi na mgao kutoka kwa serikali uliangaziwa mara ya mwisho 2018.

Hata hivyo, bei ya bidhaa na huduma imeongezeka tangu wakati huo lakini taratibu hizo zimesalia vivyo hivyo.

Gharama ya masomo na bidhaa za vyakula imezidi kupanda, hali ambayo imewalemea wasimamizi wa shule na kuwalazimu kupunguza baadhi ya matumizi.

Serikali vilevile huendesha mpango wa Elimu Msingi bila Malipo (FPE) ambao umekuwepo sasa kwa miaka 20.

Licha ya malalamishi kutoka kwa walimu wakuu, ufadhili unaotolewa kwa kila mwanafunzi umesalia Sh1,420 tangu 2003.

Ikizingatiwa idadi kubwa ya shule za msingi za umma ni za kutwa, aghalabu wazazi hugharamikia mahitaji ya masomo ya watoto wao.

Japo serikali hutoa kitabu kimoja cha kiada kwa kila somo, wazazi huhitajika kununua vifaa vinginevyo vya masomo, kama vile kalamu na madaftari.

“Hakuna elimu ya bure hapa. Unaweza ukafanya nini na Sh1,420 kwa mwaka mzima katika uchumi huu,” ahoji mzazi kutoka Nairobi kwa jina Jimmy Mwenesi.

Baadhi ya wadau wamehusisha matokeo duni katika shule za kutwa na ukosefu wa fedha na upungufu wa wafanyakazi, hali ambayo imesababisha idadi kubwa ya wazazi na wanafunzi kuepuka shule hizo na kung’ang’ania nafasi chache katika shule zilizosimamiwa vyema.

Mwaka 2023, Muungano wa Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari (Kessha) uliwasilisha pendekezo kwa Wizara ya Elimu ukiitaka iongeze karo inayolipwa na wazazi au mgao unaotolewa na serikali.

 

Wazazi na walezi wafurika kwenye maduka ya vitabu jijini Nairobi baada ya shule kufunguliwa. PICHA|BONFACE BOGITA

Kessha imependekeza nyongeza ya karo ya Sh19,628 kwa wanafunzi katika shule za kitaifa ambapo karo mpya kwa mwaka katika kitengo hiki itapanda hadi kufikia Sh73,182 kutoka Sh53,554.

“Karo inayotozwa na shule hizo haitoshi huku shule zikiendesha shughuli zake kwa kutumia bajeti yenye upungufu mno. Madeni yanalundikana shuleni huku maendeleo ya miundomsingi yakikwama,” walilalamika walimu wakuu.

Aidha, Kessha imependekeza nyongeza ya Sh25,488 kwa wanafunzi katika shule za mikoa na kaunti na Sh5,372 kwa shule za kutwa zinazojumuisha karibu asilimia 70 ya wanafunzi wa sekondari.

“Mpango wa FDSE umekumbwa na changamoto mbalimbali ambazo zimeathiri pakubwa kusudi la mpango uliodhamiriwa mema. Pana haja ya serikali kushughulikia kwa dharura changamoto na vizingiti mbalimbali ambavyo vimelemaza mpango huu,” ilisema Kessha kupitia taarifa

“Nakala hii inaangazia pendekezo la Kessha kuhusu karo inayofaa kutozwa katika shule zetu kwa kuzingatia gharama ya maisha na kuisawazisha na haja ya kupata elimu bora ya sekondari kwa bei nafuu.”

Hata hivyo, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amepuuzilia mbali uwezekano wa kuongeza karo.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Shule za Sekondari Nchini (Kuppet) Akello Misori alisema jana kuwa, serikali ni sharti itenge kiasi zaidi cha pesa kwa sekta ya elimu ili Wakenya wote waweze kupata elimu bora ikizingatiwa elimu ni haki msingi kikatiba.

“Msimamo wetu kama Kuppet; nendeni kwa umma na ufadhili elimu ya umma. Ili tufanikishe maendeleo ya Karne ya 21, serikali inahitaji kutekeleza inachoahidi. Tumekuwa tukiagiza Bunge kutengea elimu kiasi zaidi cha pesa,” alisema Bw Misori.