Hakikisho wafanyakazi 6,021 NMS wataajiriwa na serikali ya Nairobi

Hakikisho wafanyakazi 6,021 NMS wataajiriwa na serikali ya Nairobi

NA WINNIE ONYANDO

GAVANA wa Nairobi, Johnson Sakaja ameahidi kuwaajri wafanyakazi 6,021 waliokuwa chini ya Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi(NMS).

Hii ni baada ya mkurugenzi wa NMS, Mohamed Badi kurejesha majukumu ya idara hiyo kwa serikali ya kaunti ya Nairobi.Akizungumza baada ya serikali yake kurejeshewa majukumu hayo, Gavana Sakaja alisema kuwa hakuna haja wafanyakazi hao kufutwa kazi kwa kuwa serikali yake itawahitaji.Alisema kuwa watashirikiana na wafanyakazi hao ili kuwahudumia wakazi wa Nairobi.

“NMS kurudishia kwa serikali yangu majukumu hakumaanishi kuwa wafanyakazi chini ya idara hiyo wafutwe kazi. Serikali yangu itawahitaji kwa hivyo nitawaajiri wote,” akasema Bw Sakaja.

Wafanyakazi hao wa NMS walitolewa kutoka serikali ya kaunti ya Nairobi ili kuiwezesha idara hiyo kuendeleza majukumu yake.

Akizungumza na Taifa Leo, mwenyekiti wa Wafanyikazi Nairobi, Anthony Kimingi alisema wanafurahia hatua hiyo.

Alibainisha kuwa wafanyakazi hao 6,021 walitolewa kutoka idara nne zinazojumuisha Afya, Mazingira, Barabara na Makazi.

Alisema kuwa wafanyakazi hao wamepitia dhuluma mbalimbali chini ya utawala wa Bw Badi.

“Kama mwenyekiti, nina furaha kwa sababu watu wangu watashughulikiwa ipasavyo chini ya serikali ya gavana Sakaja. Tuko tayari kujiunga na wafanyakazi wengine 5,554,” akasema Bw Kimingi.

Alisema kwamba NMS imekuwa ikiwalipwa wafanyakazi mishahara kuchelewa.

“Wafanyakazi wamekuwa wakilipwa kuchelewa. Baadhi ya wafanyakazi wa NMS walipokea mishahara yao ya Agosti siku chache zilizopita,” akasema Bw Kimingi.

Kwa upande wake, Susan Akinyi, Kiongozi Msaidizi wa Wanawake, Nairobi alisema kuwa wana furaha kama muungano kujiunga na serikali ya Bw Sakaja.

  • Tags

You can share this post!

Jaji afungulia wanasiasa wasio na digrii kuwania ugavana

Korti yaamua wajane wana haki kurithi mali wakiolewa tena

T L