Habari Mseto

Hakimu aachilia washukiwa akisema 'Nimewaachia Mungu'

April 12th, 2018 2 min read

Na BRIA OCHARO

HAKIMU alishangaza waliohudhuria kesi kortini mjini Mombasa, alipowaachia Mungu washukiwa ambao hawakupatikana na hatia ya wizi wa mabavu na kumuua afisa wa polisi.

Bw Evans Makori ambaye ni hakimu mkuu, alisema kwamba washukiwa wanapaswa kujitetea mbele ya Mungu kuhusiana na madai ya makosa waliyokuwa wameshtakiwa nayo, kwa kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthitisha kesi dhidi yao.

“Ikiwa kuna mtu yeyote miongoni mwenu (watuhumiwa) ambaye alimwua afisa wa polisi, basi ajiandae kujibu maswali hayo mbele ya Mwenyezi Mungu. Ushahidi ulioletwa mbele ya mahakama dhidi ya yenu haukutosha,” akasema Bw Makori.

Jacob Chanze, Safari Nazro, Athuman Nzai, Keraga Kombe, Kazungu Charo, Jairus Kombe na wengine wanne walikuwa wameshtakiwa kwa kuhusishwa na kumwibia Koplo Athenus Kilonzo bunduki aina ya  G3 na kisha kumuua.

Mahakama ilikuwa imeambiwa kuwa watuhumiwa walimpiga afisa huyo wakiwa na mapanga, marungu, shoka na mikuki na kumnyang’anya bunduki yake.

Ilidaiwa kuwa siku hiyo, Desemba 11, 2014 katika eneo la Kinarani, kaunti ndogo ya Kaloleni, Kilifi, watuhumiwa walipokaribia kambi ya polisi ya utawala ya Kinarani wakitupa mawe, polisi walianza kufyatua risasi lakini bunduki zilikataa kufanya kazi.

Pia, mahakama iliiambia kuwa polisi watatu ambao walipata majeraha katika shambulio hilo, walikufa baadaye walipokuwa wakitibiwa hosiptalini.

Watuhumiwa walifunguliwa shtaka la ziada la kuwapiga na kuwaumiza Dominic Emoli na Sam Sora na kuwasababishia madhara ya mwili.

Emmanuel Tsui na Bw Kahindi Karisa wanashutumiwa kwa kosa la mbadala kwa kuidhinisha kiapo kwa wanachama wa Mombasa Republican Council (MRC).

Aidha, Kahindi alishtakiwa kwa kupatikana na vitu vinavyoaminika kuwa zinatumika katika mambo ya kichawi.

Akiwaachilia washukiwa, hakimu alisema upande wa mashtaka ulishindwa  kuthibitisha kesi yake, na kwamba ushahidi uliotolewa mahakamani haukutosha.
“Watuhumiwa hawakutambuliwa vizuri, taarifa za ushahidi hazikuenda sambamba na ushahidi.

Hakuna shahidi aliyeona washukiwa wakifanya makosa hayo. Kwa hiyo madai yote huendelea kuwa uvumi tu kama hayataungwa mkono na ushahidi,” alisema Bw Makori.

Hakimu huyo alimuachilia Kahindi kwa mashtaka ya uchawi, akisema kuwa hakuna mtaalamu aliyefika mahakamani kuthibitisha kuwa vifaa vilivyopatikana vilitumiwa katika uchawi.