Habari

Hakimu aamuru raia 22 wa Eritrea warudishwe kwao

May 24th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA 22 wa Eritrea waliokamatwa siku 10 zilizopita na kushtakiwa kwa kuwa nchini kinyume cha sheria Ijumaa wamemlilia hakimu mahakamani wakiomba warudishwe kwao na kudai wameteseka mno wakiwa korokoroni.

Wakizugumza kupitia kwa mkalimani washtakiwa hao walisema walitoroka nchini mwao kwa sababu ya dhiki mbalimbali na ukosefu wa ajira na walikuwa wanaenda Afrika Kusini kujitafutia riziki.

Bi Selam Braham na wengine 21 walitiwa nguvuni eneo la Juja kwenye barabara kuu ya Thika–Nairobi wakiwa wameabiri magari matatu aina ya Toyota Lexus.

Hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot alifahamishwa kuwa washukiwa nao waliingizwa nchini kwa kutumia njia za mkato wakiwa na nia ya kusafiri hadi Afrika Kusini kusaka ajira.

Washtakiwa hao waliojumuisha wanawake 12 walimsihi Bw Cheruiyot aamuru warudishwe kwao licha ya dhiki wanazokumbana nazo.

Akiamuru washtakiwa hao warudishwe nyumbani, Bw Cheruiyot alisema washukiwa hao wamekaa rumande kwa muda mrefu na kuwa haki zao zimekandamizwa.

Washtakiwa hao walikiri walikamatwa mnamo Mei 15, 2019, wakiwa nchini Kenya kinyume cha sheria za Uhamiaji.

Afisa wa Uhamiaji alimweleza hakimu hapingi washtakiwa hao wakirudishwa kwao.

“Naamuru washtakiwa wakabidhiwe ubalozi wao nchini ndipo warudishwe nchini mwao,” alisema Bw Cheruiyot.

Baada ya kuamriwa warudishwe kwa washtakiwa hao walifurahi huku wengine wakitiririkwa na machozi ya furaha licha ya ugumu wa maisha.