Habari Mseto

Hakimu afichua alipigwa kalamu kwa kuugua Ukimwi

January 7th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

HAKIMU aliyefutwa kazi kwa kumfichulia msajili mkuu wa idara ya mahakama Bi Anne Amadi alikuwa akiugua Ukimwi anaomba mahakama kuu iamuru alipwe fidia.

Hakimu  huyo aliyetimuliwa kazini 2016 anasema kuwa alikuwa ametunukiwa tuzo ya kuwa “hakimu bora zaidi katika idara ya mahakama.”

Kupitia kwa wakili Jason Okemwa (pichani) anaomba mahakama kuu iamuru alipwe fidia na mishahara yake yote tangu 2016 kwa vile alitimuliwa kazini kwa sababu ya ugonjwa licha ya madai ya Bi Amadi aliachishwa kazi kwa kuchelewesha utoaji wa maamuzi katika kesi 204.

Hakimu huyo aliyehudumia idara ya mahakama kwa miaka 17 anasema alidhulimiwa na Tume ya Kuajiri Watumishi wa Idara ya Mahakama (JSC) na Bi Amadi.

Mlalamishi anasema alipofichua amelazwa hospitali kadi za bima ya afya zilitwaliwa zote na “ kuachwa afe bila msaada.”

Alipokuwa kihudumu mlalamishi anasema kuwa anapokea mshahara wa Sh441,375 kwa mwezi.

Hakimu huyu ambaye hatuwezi kuchapisha jina lake kwa sababu ya hadhi yake na kutunza haki zake kama mgonjwa wa HIV anasema kuwa alijiunga na idara ya mahakama mwaka wa 2000 na kupandishwa cheo kutokana na bidii kazini hadi cheo cha hakimu mwandamizi.

Mlalamishi anasema alipohamishwa na kupelekwa mahakama ya Kitale, pasta wa Kanisa alipokuwa anahudhurua ibada alipendezwa naye kisha wakafunga pingu za maisha.

Anasema alipojifungua alianza kupatwa na matatizo ya kiafya hadi alipopimwa na kuelezwa ameambukizwa maradhi ya HIV.

Mahakama iliambiwa hakimu huyu alianza kuhudhuria hospitali na hata kulazwa Nairobi Hospital.

Kesi hiyo iliratibishwa kuwa ya dharura na mahakama ya kuamua kesi za viwanda.