Habari Mseto

Hakimu amhurumia aliyekiri kujuindia leseni ya kupima wagonjwa

August 24th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MUHUDUMU wa maabara ya kupima magonjwa Ijumaa alitozwa faini ya Sh30,000 ama atumikie kifungo cha miezi mitatu jela kwa kupatikana na leseni feki.

Bi Rose Njeri Kamau alitozwa faini hiyo na hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Nairobi Bw Francis Andayi alipokiri mashtaka matatu ya kupatikana amejitengenezea leseni ya taaluma.

Mahakama ilifahamishwa na kiongozi wa mashtaka Bi Kajuju Kirimi kuwa mshtakiwa hakuweza kujieleza sababu hana leseni kutoka kwa bodi ya maabara ya Serikali, KMLTTB.

“Maafisa wa polisi waliomtia nguvuni mshtakiwa walimkuta akiwa na leseni yam waka wa 2017 na 2018 na hazikuwa zimetayarishwa na bodi ya KMLTTB,” Bi Kirimi  aliambia korti.

Mahakama ilielezwa kuwa mshtakiwa alikuwa anahatarisha maisha ya wagonjwa wengi kwa vile hajahitimu na kuidhinishwa na KMLTTB.

“Kazi aliyokuwa anafanya mshtakiwa ni ya kuhatarisha maisha ya wagonjwa wanaoenda kusaka huduma za hali yao,” alisema Bi Kirimi.

Aliomba mahakama imwadhibu vikali.

Mashtaka dhidi yake yalisema kuwa alijitengenezea leseni nambari A05743 akidai imetayarishwa na kutolewa na bodi ya KMLTTB.

Shtaka lilisema muda wa kutamatika kwa leseni hiyo ni Desemba 31 2018.

“Umehitimu na taaluma ya kupima magonjwa kwa njia ya maabara,” mshtakiwa aliulizwa na hakimu.

“Ndio nimehitimu. Hata nataka kujiunga na chuo kikuu kupata shahada,” alijibu Njeri.

“Ni kweli ulikutwa na leseni hizo mbili, moja ya 2017 na nyingine ya 2018.” Bw Andayi alimwuliza mshtakiwa.

“Ndiyo, nilikutwa nazo,” alijibu Njeri.

“Mbona ulijitengenezea? Kwa nini hukuenda kufanya mtihani upewe leseni kirasmi?” hakimu alimhoji.

“Nilikuwa nahitaji pesa kwa haraka kwa vile mama yangu alikuwa mgonjwa na alikuwa amelazwa hospitali. Nilisaidiwa na mtu kupata leseni hii,” alijibu.

Aliomba msamaha.

Hakimu alimtoza faini akisema umri wake ni mdogo na ameghairi matendo yake.