Hakimu amkemea Rigathi Gachagua

Hakimu amkemea Rigathi Gachagua

NA RICHARD MUNGUTI

MWANIAJI mwenza wa kiti cha urais wa muungano wa Kenya Kwanza Rigathi Gachagua anayekabiliwa na kesi ya ufisadi wa Sh7.4 bilioni amekemewa na hakimu mkuu Victor Wakumile kwa kudai hadharani hana hatia na kwamba kesi imechukua muda mrefu kukamilika.

Na wakati huo huo Bw Gachagua hakufika mahakamani kwa vile amekumbwa na msiba wa kufiwa na nduguye mkubwa James Reriani Gachagua.

Bw Gachagua aliteuliwa na mwaniaji Urais wa Kenya Kwanza Dkt William Ruto mnamo Jumapili iliyopita.

Bw Wakumile alighadhabishwa na matamshi ya Bw Gachagua kwamba hana hatia hata!

Hakimu alisema kortini kesi ya ufisadi wa zaidi ya Sh7.4 bilioni haijaanza kusikilizwa ilhali “taarifa zilitangazwa na chombo kimoja cha habari kikimnukuu Gachagua akisema hana hatia.”

“Hii kesi haijaanza kusikilizwa hata! Na nilishangaa kusoma katika mojawapo ya magazeti mshtakiwa hana hatia,” akasema Bw Wakumile.

Bw Wakumile alisema endapo Bw Gachagua aliye pia Mbunge wa Mathira anataka kujiondolea lawama mwenyewe basi itabidi atwae hatamu za uhakimu na kusikiliza kesi hiyo kisha atoe uamuzi.

Wakili Gibson Kimani anayemwakilisha Bw Gachagua alieleza mahakama mshtakiwa hakufika mahakamani kwa vile anaandaa mazishi ya nduguye mkubwa.

Bw Kimani alimkabidhi hakimu cheti cha mazishi na tangazo la kifo la nduguye mshtakiwa kisha akaomba mahakama itengee kesi hiyo siku nyingine ya kusikilizwa.

Kiongozi wa mashtaka Bw Willy Momanyi hakupinga ombi la kesi hiyo kuahirishwa ila aliambia korti tayari nakala za mashahidi na ushahidi wote umekabidhiwa kwa mwanasiasa huyo.

Bw Momanyi alisema mashahidi 40 watafika kortini kusimulia jinsi Sh7.4 bilioni zilivyoporwa kwa njia ya ufisadi.

Bw Gachagua ameshtakiwa pamoja na msimamizi wa hazina ya kufadhili maendeleo eneo la uwakilishi bungeni la Mathira Bw William Mwangi Wahome, Ann Nduta Ruo, Jullianne Jahenda Makaa and Samuel Murimi Ireri, Grace Wambui Kariuki, Lawrence Kimaru, Irene Wambui Ndigiriri, David Reuben Nyangi Nguru na kampuni yake Rapid Medical Supplies Ltd.

Wote tisa wameshtakiwa kwa kula njama za kuilaghai kaunti ya Nyeri mabilioni hayo ya pesa kwa madai waliinunulia hospitali kuu ya kaunti hiyo mashine ya kusafisha figo.

Bw Wakumile alitenga Septemba 5, 2022 siku ya kusikilizwa kwa kesi hiyo ya ufisadi.

Pia aliwataka washtakiwa wawe na uzoevu wa kuzungumza kupitia kwa mawakili wao.

Washtakiwa wako nje kwa dhamana.

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Saladi ya kuku, jibini na vipande vya...

Kocha wa Kangemi Allstars asema heri kuvuna alama moja...

T L