Hakimu ashuku ipo njama kuchelewesha kesi ya ufisadi dhidi ya Jumwa

Hakimu ashuku ipo njama kuchelewesha kesi ya ufisadi dhidi ya Jumwa

Na PHILIP MUYANGA

MAHAKAMA ya kusikiliza kesi za ufisadi imelalamikia mienendo ya mawakili wa Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa na washukiwa wengine sita, ikishuku wanataka kuchelewesha kesi kusudi.

Hakimu Mkuu wa mahakama ya Mombasa, Bi Edna Nyaloti, amewataka mawakili Jared Magolo, Danstan Omari, Shadrack Wambui na Titus Kirui wafike mbele yake, huku upande wa mashtaka ukilalamika kuwa wanatumia vibaya mahakama.

Bi Nyaloti alisema licha ya mawakili hao kusema wamejiondoa katika kesi, aliwaona wakichungulia mahakamani wakati washtakiwa walipokuwa wakijibu upya mashtaka yao.

“Kuna wakati hufika ambapo ni lazima mahakama ichukue hatua,” akasema Bi Nyaloti, kabla kuagiza mawakili hao wanne wafike mbele yake.

Mawakili hao walijiondoa Jumatatu wakati upande wa mashtaka ulipofanya marekebisho madogo katika hati ya mashtaka ya ufisadi yanayomkumba Bi Jumwa na wenzake.

Hatua hiyo ya hakimu ilitokea baada ya upande wa mashtaka kupinga ombi la wakili mpya wa Bi Jumwa na washtakiwa wenzake, Bw Duncan Osoro, ambaye aliomba kesi iahirishwe.

“Sijapewa stakabadhi za kesi hii ndiposa naomba iahirishwe. Nahitaji muda zaidi,” akasema.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa Bw Osoro alikuwa ameonekana akizungumza na washtakiwa na mawakili wao wa awali nje ya mahakama kwa hivyo ombi lake halikuwa na msingi.

“Mahakama hii inafaa ikomeshe jinsi wengine wanavyoitumia vibaya. Vitimbi hivi vitaendelea hadi lini?” akasema kiongozi wa mashtaka, Bw Alex Akula.

Bw Osoro alisema alipozungumza na mawakili hao alikuwa anawaomba wamkabidhi stakabadhi, lakini hataweza kujiandaa kuendelea na kesi hiyo kwa siku moja pekee ilhali upande wa mashtaka umekuwa na stakabadhi hizo kwa takriban miaka miwili ikijiandaa.

Bi Jumwa alishtakiwa kwa madai ya kushiriki katika njama ya ufisadi wa Sh19 milioni zilizolipwa kwa kampuni ya Multiserve kupitia kwa zabuni nambari MLD/NG-CDF/01/2017/2018 iliyotolewa na afisi ya CDF ya Malindi.

Washtakiwa wenzake ni Wachu Omar, Kennedy Otieno, Bernard Riba, Sophia Saidi, Margaret Kalume, Robert Katana na kampuni ya Multiserve.

Imedaiwa kuwa kitendo hicho kilitokea kati ya Mei 14 na Oktoba 12, 2018 katika Kaunti Ndogo ya Malindi, Kaunti ya Kilifi.

You can share this post!

Kingi asalimu amri kuvuliwa cheo ODM

World Rugby yapongeza Mkenya Humphrey Kayange kuingia...