Hakimu asimulia jinsi walivyoponea shambulio

Hakimu asimulia jinsi walivyoponea shambulio

NA STEPHEN ODUOR

HAKIMU Mkuu Mwandamizi wa Mahakama ya Garsen, Paul Rotich, ambaye ni miongoni mwa maafisa watano wa mahakama ya Garsen walionusurika shambulio la kigaidi amesimulia masaibu waliyopitia walipovamiwa na al-Shabaab.

Maafisa hao wa mahakama walishambuliwa na magaidi katika eneo la Lango La Simba jioni jioni ya Januari 26.

Walikuwa wanatoka kwenye mkutano katika kijiji cha Kipini, Kaunti ya Tana River, kabla ya kuvamiwa.

“Tulikuwa tunazungumza tu jinsi siku hiyo ilivyokuwa na mafanikio na mbele yetu kulikuwa na lori. Ghafla kundi la watu waliokuwa na silaha walitokea msituni na kufuata gari letu,” alisimulia.

Bw Rotich anasema kuwa walidhani watu hao waliokuwa na silaha walikuwa maafisa wa usalama wa kushika doria katika barabara hiyo. Walikuwa wamevalia nguo za kijeshi, buti, vivuli, na kilemba cha Arafat.

Afisa wa polisi aliyekuwa akiwasindikiza alipoona bunduki zao ambazo si sawa na zinazotumiwa na maafisa wa usalama, alimtaka dereva kuongeza kasi.

“Walipoona dereva wetu anaongeza kasi, walirusha guruneti lakini kwa bahati nzuri halikutupata. Hapo ndipo walitufyatulia risasi,” akasema.

Risasi zilipozidi, dereva alisimamisha gari na kila mmoja akatoroka kujiokoa licha ya baadhi yao kujeruhiwa.

Muda mfupi baadaye, wanajeshi walitokea na kujibu mashambulio na makundi hayo mawili yalikabiliana kwa risasi na kurushiana vilipuzi kwa dakika kadhaa. Makabiliano hayo yalitibua azma ya magaidi hao kutaka kuangamiza maafisa wa mahakama.

Wanamgambo hao wa al-Shabaab walitoweka na kisanduku kilichokuwa na stakabadhi za mahakama na funguo za gari.

“Wapikanaji walipokimbia, wanajeshi walikuja msituni kututafuta. Awali, tulidhani walikuwa magaidi ambao walitaka kutuua. Lakini mmoja wa wanajeshi alijitambulisha na kuzungumza nasi kwa lugha ya Kiswahili ndipo tuliamini,” Bw Rotich aliambia Taifa Leo.

Kulingana na Bw Rotich, mwendesha mashtaka alijeruhiwa kwa risasi kichwani.

Anasema kuwa maafisa wa mahakama wamekuwa wakienda katika eneo la Kipini kusikiliza na kuamua kesi kuhakikisha kuwa wakazi wanapata haki.

Shambulio hilo limezua maswali ikiwa lilihusiana na kesi zilizokuwa zikishughulikiwa na maafisa hao au la.

Tukio hilo huenda likasababisha wakazi wa eneo la Kipini kusafiri umbali mrefu kwenda kutafuta huduma za mahakama mjini Garsen.

“Tulikuwa tumepiga hatua katika upatikanaji wa haki, kilichotokea kinaweza kudhibitiwa kwa kuweka ulinzi mkali kwenye barabara hiyo, ili kuhakikisha watu wa Kipini hawahangaiki,” anasema.

Wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu sasa wanataka serikali kuongeza ulinzi kwa maafisa wa mahakama ili kuepuka kutatizika upatikanaji wa haki katika Kaunti ya Tana River.

Meneja wa shirika la Upatikanaji wa Haki la Access to Justice Stephen Otoi alitaja shambulio hilo dhidi ya maafisa wa mahakama kuwa la kuogofya.

“Kaunti ya Tana River na kila mtu hawezi kufika kortini kutokana na umbali mrefu. Kuna haja kwa serikali kuchukulia kwa uzito suala la usalama wa mafisa wa mahakama,” akasema.

Bw Otoi pia anasema kuwa maafisa wa serikali katika Kaunti za Lamu na Tana River wamekuwa wakilengwa na magaidi hivyo wanafaa kupewa ulinzi mkali ili waendelee kutekeleza majukumu yao.

  • Tags

You can share this post!

Kiboro arai viongozi kuhubiri amani

Kingi aonya wakazi dhidi ya kuuza ardhi na kubakia maskwota

T L