Habari

Hakimu katika kesi ya Waititu ajiuzulu

June 14th, 2019 1 min read

Na BENSON MATHEKA na SAM KIPLAGAT

HAKIMU Mkazi wa Mahakama ya Kiambu Brian Khaemba amejiuzulu Ijumaa saa chache baada ya kusimamishwa kazi kwa kutumia vibaya mamlaka ya afisi yake katika kesi ambayo Gavana wa kaunti hiyo Ferdinand Waititu anachunguzwa kwa madai ya ufisadi.

Hakimu huyo ambaye mwezi jana alitoa agizo tata la kumuachilia kwa dhamana Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu kabla yake kufunguliwa mashtaka, alikana kufanya kosa lolote akisema alifuata uamuzi wa Mahakama Kuu alioutaja kwenye agizo lake.

Alikana madai kuwa alishughulikia ombi la dhamana ya Waititu licha yake kuwa kwenye likizo ya kuwa mgonjwa, akisema kuwa kesi hiyo iliwasilishwa kwake na Hakimu Mwandamizi Stella Atambo.

“Nilivyosema kwenye barua yangu ya Juni 13, nilishughulikia ombi hilo kufuatia agizo la Hakimu Mwandamizi Mheshimiwa Stella Atambo, ambaye ndiye alikuwa akisimamia maombi yote ya dhamana. Mheshimiwa Atambo hajakana hilo,” alisema Bw Khaemba katika jibu alilotoa Juni 14.

Kujipatia riziki

Hakimu mkazi huyo alisema kuwa kutokana na ukosefu wa muda wa kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi yake ya nidhamu, na kwamba Jaji Mkuu David Maraga alikuwa amemsimamisha kazi bila mshahara wowote, alisema aliamua kujiuzulu ili kusaka njia zingine za kujipatia riziki.

“Baada ya kubaini athari za barua hiyo ya kunisimamisha kazi, hususan suala la kutolipwa mshahara wowote na kwamba kesi hiyo ya nidhamu haina tarehe ya kikomo, nimewasilisha barua ya kujiuzulu ili niweze kutafuta mbinu zingine za kupata mapato,” alieleza Bw Khaemba.

Jaji Mkuu Maraga alikuwa ameagiza Khaemba kutoa majibu kwa Tume ya Mahakama (JSC).