Hakukuwa na wizi wa KCSE, Machogu ajibu

Hakukuwa na wizi wa KCSE, Machogu ajibu

Na ESTHER NYANDORO

WAZIRI wa Elimu Ezekiel Machogu amefichua kuwa shule za upili za Mang’u na Alliance ndizo ziliongoza kwa idadi ya watahiniwa wa KCSE ambao walipata alama A zikiwa na wanafunzi 82 na 72 mtawalia.

Bw Machogu wakati huo huo alikanusha vikali kuwa kulikuwa na udanganyifu katika mtihani wa KCSE wa 2022 ambao matokeo yake yalitolewa wiki jana.

Alikuwa akizungumza katika Taasisi ya Ukuzaji Mitaala Nchini (KICD) Nairobi baada ya kuzindua shughuli za usambazaji wa vitabu vya Gredi ya Saba katika Shule za Sekondari za kiwango cha chini.

“Nimeona kuna habari za uongo ambazo zinasambazwa. Watu wanasema kuwa tuliwatoa wanafunzi wengi sana ambao wana alama ya A. Huu ni uongo kutoka kwa watu ambao hawapendi ufanisi wa wanafunzi wetu,” akasema Bw Machogu.

Waziri huyo aliongeza kuwa mnamo 2021 kulikuwa na wanafunzi 1138 ambao walipata alama ya A na mnamo 2022 idadi hiyo ilipanda kidogo kwa kuwa walikuwa wanafunzi 1146.

Aliongeza kuwa hakuwa na sababu yoyote ya kumyima mwanafunzi aliyepata alama A ilhali walikuwa wametia bidii na walistahili.

Pia alijitetea akisema idadi ya wanafunzi ambao walipata alama ya C+ na zaidi na kuhitimu kuingia chuo kikuu ilipanda kwa asilimia mbili pekee kutoka 17.49 hadi 19.03.

“Hakuna mabadiliko makubwa ukilinganisha jinsi wanafunzi walivyofanya kwenye mtihani wa KCSE wa 2021 na 2022. Idadi ya wanafunzi ambao walifuzu kuingia chuo kikuu bado ipo chini ya viwango vya kimataifa vya asilimia 30. Kwa hivyo, hakuna sababu zozote za kilio kuwa mtihani uliibwa,” akasema.

Vilevile, Bw Machogu aliwataka Wakenya wakome kutumia matokeo hayo kukejeli jamii moja akisema kuwa ukanda wa Nyanza anakotoka, wanafunzi wengi waliopata alama ya A walitoka Siaya na idadi yao ilikuwa 72.

Waziri huyo alisema Migori ilifuata kwa wanafunzi 66 waliopata alama ya A, Kisumu (59), Kisii (50), Homa Bay (47) na katika Kaunti ya Nyamira ni wanafunzi 31 ndio walipata A.

Akigusia kung’aa kwa Shule ya Upili ya Nyambaria kwenye mtihani huo, alisema matokeo hayo yalitokana na uongozi bora chini ya usimamizi wa mwalimu mkuu Boaz Owino ambaye alihamishwa kutoka Maranda High inayopatikana Siaya.

Bw Owino alistaafu mnamo Disemba mwaka uliopita.

“Si miujiza bali kiini cha kung’aa kwa Nyambaria kilitokana na uongozi wa kuridhisha,” akasema.

Waziri huyo pia aliwaonya Wakenya wakome kutumia mitandao kueneza uvumi kuhusu masuala ya elimu na wale ambao wana ushahidi kuwa KCSE iliibwa wawasilishe ushahidi huo.

“Vigezo vya kufuta matokeo kutokana na udanganyifu ni juu sana. Hakuna ushahidi kuwa mtihani uliibwa na kusababisha niwaadhibu watahiniwa,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Kiongozi wa IS auawa nchini Somalia

DARUBINI YA WIKI, Januari 29, 2023  

T L